Dar es Salaam. Wakati Serikali ikihangaika kutafuta ‘mwarobaini’ wa vifo vya wanawake wajawazito wanapojifungua, imebainika kuwa kuna idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wake (njiti), ambao hufariki dunia kila siku katika hospitali mbalimbali nchini kutokana na kukosa huduma.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika
hospitali mbalimbali za Serikali jijini Dar es Salaam na mikoani,
umebaini kuwa baadhi ya watoto hao hupoteza maisha kutokana na
kukosekana kwa mashine maalumu za kuwahifadhia zijulikanazo kama
‘Incubator’.
Kwa mujibu wa Shirika la Mama Ye! Linalojihusisha
na afya ya mama na mtoto, linasema kuwa kila mwaka watoto 210,000
huzaliwa kabla ya kutimiza muda wake, ambapo kati yao watoto 13,900
hufariki dunia, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya 12 kwa kuwa na
idadi kubwa ya watoto njiti duniani.
“Watoto wanaozaliwa mapema wana uwezekano wa mara
sita hadi 26 kufariki dunia katika wiki nne za kwanza, ukilinganisha na
watoto wanaozaliwa katika muda wake,” inasema sehemu ya ripoti ya Mama
Ye!
Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto na wanawake
katika shirika hilo, Dk Moke Magoma anasema wanaume pia wanamchango
mkubwa katika kuwaokoa watoto njiti, kwani wanaweza kuwasaidia wake zao
kuwaweka watoto vifuani ili wapate joto.
Alitoa mfano, daktari huyo anasema kuwa mwaka 2012
mwanamume mmoja mjini Zanzibar, aliokoa maisha ya mtoto wake kwa
kumweka kifuani na kisha kumfunga kwa nguo baada ya mke wake kujifungua
watoto mapacha njiti.
Hata hivyo, ripoti ya mwaka 2014 iliyotolewa na
Shirika la Save the Children, watoto 36, 528 hupoteza maisha kila mwaka
siku moja kabla ya kuzaliwa.
Watoto njiti milioni 15.1 huzaliwa kila mwaka duniani kote, idadi ambayo inamaanisha kuwa mtoto mmoja kati ya 10 huzaliwa njiti.
“Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa watoto
wa kiume wana asilimia 14 ya kuzaliwa njiti ikilinganishwa na wa kike,
hata hivyo, watoto wa kike wanauwezekano mkubwa wa kufariki dunia kuliko
wa kike kutokana na lishe duni,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inasema kuwa mtoto njiti ambaye
hufanikiwa kuishi husumbuliwa na matatizo ya muda mrefu kama uono
hafifu, kutokusikia ipasavyo na maradhi sugu ya mapafu.
Katika Hospitali ya Amana, Wilaya ya Ilala, zaidi
ya watoto njiti 60 huzaliwa kwa mwezi (sawa na asilimia 13 ya watoto
wote), ambapo Februari mwaka huu jumla ya watoto 467 walizaliwa wakiwa
na matatizo mbalimbali ya kiafya.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni
hospitalini hapo, Daktari Bingwa wa watoto, Dk Mtagi Kibatala anasema
kuwa zaidi ya wajawazito 70 hujifungua kila siku katika hospitali hiyo,
idadi ambayo ni sawa na watoto 2,100 kwa mwezi na 25,200 kwa mwaka.
Source :Mwananchi leo
Na Mjmbe jr
Mbeya.
Source :Mwananchi leo
Na Mjmbe jr
Mbeya.
Post a Comment