Rais Jakaya Kikwete akiwa ameongozana na ujumbe mzito wa marais na mawaziri wakuu wastaafu wa pande mbili za Muungano, leo atalihutubia na kulizindua Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, kulingana na Kanuni ya 75 (1) ya Bunge hilo.
Uamuzi wa kuambatana na viongozi wastaafu wa kitaifa unatafsiriwa na wengi kama ishara ya kuupa uzito mchakato wa Katiba Mpya na uhalali wa kisiasa na kuleta umoja na utengamano miongoni mwa makundi ya wajumbe wanaounda Bunge hilo la kihistoria.
Suala la hotuba ya Rais Kikwete limekuwa mjadala katika Bunge hilo, kutokana na baadhi ya wajumbe kuhoji sababu za Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni juzi kabla ya Rais kuzindua Bunge kama Kanuni zinavyoelekeza.
Itakumbukwa kwamba mjadala huo ulizua mtafaruku baada ya baadhi ya wajumbe kumzuia Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo Jumatatu iliyopita hadi kilipofanyika kikao cha maridhiano usiku wa siku hiyo na kufikia mwafaka kwamba Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba awasilishe Rasimu hiyo juzi na Rais ahutubie Bunge leo.
Mabishano hayo yalitokana na baadhi ya wajumbe kujenga dhana kwamba ukiukwaji huo wa Kanuni ulilenga kumpa Rais fursa ya kujibu mapigo na kupangua hoja za Jaji Warioba kutokana na wajumbe wengi wa chama chake cha CCM kuonyesha wazi kupinga na kubeza mapendekezo nyeti yaliyomo kwenye Rasimu hiyo, ambayo Jaji Warioba aliiwasilisha bungeni kwa ufasaha, umakini na ustadi mkubwa kiasi cha kuwafungua macho wengi, hasa pale alipowafafanulia mambo mengi ambayo wamekiri walikuwa hawayafahamu wala kuyaelewa.
Tunaupongeza uongozi wa Bunge na wajumbe wote kwa jumla kwa kutumia busara na kuendelea na shughuli za Bunge ambazo zilikuwa zimesimama. Vinginevyo, Bunge lingesambaratika na kufuta ndoto za wananchi za kupata Katiba Mpya inayokubalika kwa wengi. Hata hivyo, mtafaruku huo ulitoa somo kwa uongozi wa Bunge kwamba Bunge hilo lisipoendeshwa kwa kufuata na kuheshimu Kanuni zilizowekwa, litasambaratika.
Pamoja na kutoa pongezi hizo, tungependa kumshauri Rais Kikwete atambue kwamba leo atakuwa akilihutubia Bunge ambalo wajumbe wake wamegawanyika, hasa kutokana na msimamo wa CCM wa kuvikataa vifungu muhimu vya Rasimu ya Katiba. Tunasema hivyo baada ya viongozi na wajumbe wengi wa CCM kutoa kauli za kuendeleza misimamo mikali inayokinzana na maoni yaliyotolewa na wananchi na kuingizwa kwenye Rasimu hii ya Katiba.
Hotuba ya Rais inaweza kugusia maudhui yaliyomo katika Rasimu ya Katiba, lakini tunadhani kufanya hivyo itakuwa kosa kubwa kwa kua atakuwa ameingia katika mtego wa kujibu hoja zilizomo katika hotuba ya Jaji Warioba aliyoitoa juzi bungeni. Akifanya hivyo atakuwa analiingiza Bunge katika sintofahamu itakayolisambaratisha, kwani yeye si sehemu ya Bunge, bali atakwenda pale kama mkuu wa nchi.
Kwa maana hiyo, hatutarajii alihutubie Bunge kuelezea misimamo yake binafsi au misimamo ya chama chake cha CCM au kundi jingine lolote lile.
Hivyo, atafanya vyema iwapo atakwenda pale kama kiunganishi muhimu cha makundi yote yaliyo bungeni. Tunadhani umoja, utengamano na nia ya serikali yake kuhakikisha Katiba Mpya inayokubalika kwa wengi inapatikana katika muda uliopangwa ndio mambo muhimu na ambao utalinusuru Bunge la Katiba.
Chanzo:Mwananchi
Mjumbe
Post a Comment