Katika kuamini kwangu juu ya uwepo wa Serikali Tatu, hivyo basi, uwepo wa Tanganyika, naamini ni katika kuchangia kuwepo kwa Muungano usiokuwa na maswali mengi huko tuendako, hivyo basi, muungano usio na kero hata za kuundiwa wizara.
Maana, hatupaswi kujenga hoja juu ya Katiba kwa kujiangalia sisi wenyewe kwa leo yetu, na labda kesho tu.
Tuwafikirie watoto wetu na vizazi vyao. Hata kama leo tutafunika kombe mwanaharamu apite, kwa muundo huu wa sasa wa Muungano wa Nchi Mbili wenye Serikali Mbili badala ya Moja, kwamba nchi moja iliyoungana na mwenzake imebaki na nchi yake na serikali yake, ni lazima kuna watakaokuja kuhoji. Maana, utaonekana ni Muungano wa ajabu sana.
Na tatizo la kesho na keshokutwa ni walioshuhudia huo Muungano hawatakuwepo, na sababu na mazingira ya aina ya Muungano huo hazitaonekana za msingi kwa wakati huo.
Hivyo, tuispofanya sasa kazi ya kuandaa misingi imara ya Katiba yetu inapohusu muungano wetu, basi, kuna hatari kubwa ya watu wetu, kwa vizazi vijavyo, kuja kuumizana na hata kuchinjana kwa makosa tunayoyafanya leo.
Hii ni Nchi yetu sote. Na maisha tunayoishi hapa duniani ni mafupi sana. Tuna lazima ya kuitafuta fimbo sasa, kumwua nyoka mwenye sumu na huku tukijua kuwa ana sumu. Ni busara kufanya hivyo kabla ya kusubiri nyoka mwenye sumu aingine vyumbani mwetu na kuja kuwadhuru watoto wetu na vizazi vyao.
Na kibaya katika kuifanya kazi hii ni pale hofu inapotangulia badala ya kile tunachokiamini. Ndio, mwanadamu ni kiumbe mwepesi kuingiwa na kutawaliwa na hofu. Kwa mwanadamu kuna hofu anayojengewa. Hofu anayopandikzwa na hata hofu ya kujipandikizia mwenyewe.
Na wakati mwingine ni kwa kuhofia tu kuwa fikra zake hazitempendeza mwanadamu mwenzake. Hivyo, hofu yaweza kuwa ni ya kupoteza fursa na hata ajira yake. Na kosa kubwa kwa mwanadamu ni pale anapokosa ujasiri hata wa kufikiri mwenyewe kwenye yale ya msingi yenye kumhusu yeye na nchi yake aliyozaliwa.
Hivyo, mbele ya unafiki unaotangulizwa na mwanadamu nyuma yake kumejificha hofu. Na hakika, kwenye mambo ya msingi yenye kuhusu mustakabali wa nchi tuliyozaliwa hatupaswi kabisa kutoa maoni yetu yasio ya dhati ya moyoni bali unafiki.
Maana, unafiki ni UONGO. Na kuiongopea nchi uliyozaliwa kwenye jambo lenye kuhusu uhai wa nchi ni sawa na kumwongopea mama yako aliyekuzaa kwenye jambo lenye kuhusu uhai wa mama aliyekuzaa. NI DHAMBI KUBWA. NI LAANA KUU.
Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
0754 678 252(P.T)
MJUMBE Sr
Post a Comment