0Dar es Salaam. Wanafunzi wa shule zote za msingi na sekondari mkoani Dar es Salaam, wanatarajiwa kupewa chanjo ya maambukizi ya Homa ya Ini ‘Hepatitis B’, kama njia mbadala ya kukabiliana na kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo nchini
Takwimu zilizotolewa na benki ya damu zinaonyesha kuwa,asilimia 0.6 ya damu inayokusanywa hukutwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU), huku asilimia 7 ikikutwa na maambukizi ya homa ya ini , hivyo kufanya gonjwa hilo kuwa tishio jipya nchini.
Akizungumza jana, wakati wa uzinduzi wa kampeni
hiyo katika Hospitali ya Rufaa Amana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
Saidi Meck Sadiki alisema, wanafunzi na wafanyakazi wa hospitali
watapewa kipaumbele katika zoezi hilo litakalotekelezwa mwaka huu.
“Homa ya ini ni ugonjwa hatari mno, tutaanza na
kushughulika na wanafunzi wote wa shule za sekondari na msingi. Watoto
waliofanikiwa kupata chanjo hii ni waliozaliwa kuanzia mwaka 2008. Pia
tutaangalia watumishi katika hospitali zetu, naagiza hili lifanyike,
Amana wameshapimwa na kuchanjwa, naagiza Temeke, Mwananyamala na
Muhimbili wafanye hivyo, kisha hospitali binafsi pia,” alisema Meck
Sadiki.
Alisema zoezi hilo ni endelevu na kuwataka
wananchi kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya vipimo. Kaimu Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Magembe alisema ugonjwa wa homa
ya ini unakuwa tishio jipya nchini, baada ya VVU kwa miaka 25 iliyopita.
Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS),
Dk Efesper Nkya, alisema takwimu za mpango huo zinaonyesha kupanda kwa
kiwango cha homa ya ini huku VVU vikipingua. “Tumegundua hakuna
uhamasishaji kuhusu tatizo hili,” alisema Nkya.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana Dk Meshack
Shimwela alisema kampeni hiyo pia itawahusisha wanafunzi wa Vyuo Vikuu
mkoani Dar es Salaam, wahudumu wa nyumba za wageni na wanaofanya
biashara ya kujiuza.
Source:Mwananchi
Na Mjumbe Jr
Mbeya
Post a Comment