Makubaliano ya kimataifa yanamtia hatiani nahodha pale meli inapopata ajali. Chombo na watu wote wanatakiwa wafike salama na iwapo itakuwa kinyume, nahodha atashtakiwa.
Korea Kusini. Kutokana na uchungu alionao, haisikii mvua kubwa inayomnyeshea na upepo mkali unaoupiga mwili wake. Christine Kim amesimama ufukweni mwa bahari kwa zaidi ya saa tisa huku machozi yakimtiririka.
“Ndani ya yale maji meusi ya bahari yupo mtoto wangu,” anasema akionyesha kidole baharini.
Kim ni mwalimu wa Kiingereza katika kituo binafsi. Alikuwa akifundisha baadhi ya wanafunzi waliokuwa ndani ya kivutko cha Sewol kilichozama wiki iliyopita… pia alikuwamo mtoto wake wa kike.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini mpaka kufikia Jumatatu ilithibitika kuwa watu 20 wamefariki dunia na wengine 276 walikuwa bado hawajapatikana. Tangu Alhamisi ya wiki iliyopita, ndugu wa abiria waliokuwa ndani ya kivuko hicho waliweka kambi Bandari ya Paeng Mok iliyo umbali wa kilomita 20 kutoka mahali ilipopinduka meli hiyo. Kim na watu wengine wamejiinamia, kila mmoja akiomba kwa namna yake.
“Siwezi kulala kila nikimfikiria binti yangu ndani ya maji meusi na baridi kali. Siwezi kuisamehe nafsi yangu kwa sababu binti yangu alikataa kuondoka lakini nilimlazimisha,” anasema Kim.
Nahodha kukimbia meli
Sheria za usafiri wa majini zinamtaka nahodha wa meli na wafanyakazi wengine kuwa wa mwisho kutoka pale inapotokea ajali na kulazimika kutoka ndani ya chombo wanachosafiria.
Lakini miaka ya hivi karibuni matukio mbalimbali ya ajali za baharini, manahodha huwa wanakuwa watu wa kwanza kutoka mara baada ya kutokea ajali
HMS Birkenhead aliyekuwa nahodha wa meli ya Uingereza mwaka 1852 alisababisha kuwekwa kwa sheria hizo za usalama majini. Wakisafiri na meli hiyo ilianza kuzama lakini aliwaamuru wafanyakazi wenzake kuhakikisha watoto wanatolewa kwanza, kisha wanawake na wenye mahitaji maalumu.
Zoezi hilo lilifanikiwa lakini yeye na baadhi ya wafanyakazi hawakufanikiwa kutoka… walikufa maji na maiti zao hazikupatikana.
Ushujaa mwingine ulifanywa na nahodha wa meli ya Titanic, Edward J Smith ambaye alifanya juhudi kuhakikisha abiria wanatoka salama lakini alifanikiwa kuwaokoa wachache. Yeye pamoja na abiria wengine zaidi ya 1,500 walipoteza maisha.
Nahodha Lee Joon-seok wa meli ya Sewol, iliyozama hivi karibuni Korea Kaskazini amekosolewa kwa kutoka mapema ndani ya meli na kuwaacha abiria bila msaada
Chanzo:Mwananchi
Na Mjumbe Jr

Post a Comment