Unknown Unknown Author
Title: MBONA MSETO INAOTULISHA CCM NI MCHUNGU
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
MAMBO mawili yanawashughulisha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba huko Dodoma. Yote mawili yanaugusa uhalali wa kisheria wa Muungano baina y...


MAMBO mawili yanawashughulisha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba huko Dodoma. Yote mawili yanaugusa uhalali wa kisheria wa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar.


La kwanza linaihusu Hati ya Muungano.La pili linahusu idhini,iwapo Wazanzibari waliuidhinisha Muungano.


Kuhusu Hati ya Muungano kuna wanaotaka kuiona Hati hiyo, tena wanataka kuiona nakala asilia. Utata mkubwa umezuka kuhusu Hati hiyo na kadhia hiyo ni moja ya vitendawili vya Muungano wa Tanzania.


Hati hiyo ni mkataba wa kimataifa baina ya nchi mbili zilizokuwa huru, yaani Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hizo ni jamhuri zilizokuwa wanachama wa Umoja wa Mataifa, kila moja ikiwa na kiti chake katika Baraza Kuu la Umoja huo. Ni jamhuri mbili zilizokuwa na haki na hadhi sawa kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa.


Kuna wenye kusema kwamba Hati ya Muungano iko Zanzibar. Wengine wanasema iko Dar es Salaam. Wengine wanasema iko Umoja wa Mataifa licha ya Umoja huo kulikanusha dai hilo.


Wengine wanasema kuwa Salim Rashid, aliyekuwa Katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, alikuwa nayo na ameichana kwa sababu haupendi Muungano. Yeye ameniambia kwamba huo ni “uzandiki” mtupu.


Kuhusu suala la idhini ya Wazanzibari, yaani iwapo Muungano uliidhinishwa na Baraza la Mapinduzi, chombo cha utungaji sheria cha wakati huo Aprili 1964, Salim Rashid anasema “la” haukuidhinishwa na Baraza hilo. Anaongeza kwa kuhoji kwamba kwa vile Baraza la Mapinduzi halikuwahi kupitisha sheria ya kuuidhinisha Muungano basi Muungano hauna uhalali wa kisheria na kwamba sasa ndiyo Chama Cha Mapinduzi (CCM)kinajaribu kuuhalalisha.


Kwa namna mambo yanavyoendelea Dodoma inaonyesha kwamba kuna njama za kulipokonya Bunge la Katiba uhuru na uadilifu wake. Nasema hivi kwa sababu CCM inahisi ya kwamba kwa vile ina idadi kubwa ya wajumbe bungeni inaweza kufanya itakacho na kuwalazimisha wajumbe wake waufuate msimamo wa chama chao.


Tusisahau kuwa mchakato wa Katiba ulipoanza tuliambiwa kwamba zoezi hilo linazihusu nchi mbili zinazounda Muungano wa Tanzania, yaani Tanganyika na Zanzibar. Na ndiyo maana katika Tume ya Katiba, iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, nchi hizo mbili zilikuwa na uwakilishi sawa wa wajumbe 15 kutoka kila upande.


Pia Marais wawili — wa Tanzania na wa Zanzibar — waliwajibika kwa sheria kushauriana na kukubaliana juu ya hatua kadhaa za zoezi hilo la utungwaji Katiba.


Bunge la Katiba si pahala pa vyama vya siasa kufanya mapatano ya “nipe, nikupe”. La. Bunge hilo ni jukwaa ambapo wawakilishi wa Tanganyika na wa Zanzibar wakiwa washiriki wenye haki sawa katika Muungano wanatakiwa wayajadili mapendekezo makuu ya Rasimu ya Katiba ya Tume ya Warioba, hasa pendekezo kuhusu muundo wa Muungano.


Bunge hilo linakabiliwa na masuala kadhaa. Lakini lililo muhimu na lenye kuwagawa vibaya wajumbe wake ni hilo la muundo wa Muungano: iwapo muundo huo uwe wa serikali mbili au tatu. Kwa mujibu wa Warioba zaidi ya asilimia 60 ya Wazanzibari wanataka Muungano wa Mkataba ambao utaipa Zanzibar “mamlaka kamili”. Matamshi hayo yana maana ya kwamba wengi wa Wazanzibari wanadai zaidi ya ule muundo wa Muungano wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Warioba.


Suala hilo la muundo wa Muungano, kama nilivyosema, limeligawa vibaya sana Bunge la Katiba na limewasababisha wajumbe wa Bunge hilo, hasa wale watokao CCM, wafanye mambo ya ajabuajabu, yakiwa pamoja na viroja, vichekesho na kashfa. Mengine waliyoyafanya yalikuwa si ya utovu wa nidhamu tu bali hata wa adabu.


Katika zama hizi za uwazi, ilishangaza kusikia kuwa wajumbe wa CCM wamekuwa wakijaribu kutaka hata maneno “uwazi” na “uwajibikaji” yafutwe. Na wao pia wamekuwa safu ya mbele kutaka kujinyima wao na wajumbe wenzao haki ya kupiga kura kwa siri.


Mimi sina tabia ya kutabiri na ninapotabiri basi naweza tu kutabiri yaliyopita si yajayo. Lakini kwa hili nathubutu kusema kwamba ikiwa mambo katika Bunge la Katiba yataendelea kuwa shaghalabaghala kama hivi yalivyo basi Watanzania hawatopata Katiba mpya itayoyaridhia matakwa ya wengi wao. Wala hawatoweza kuipata demokrasia ya kikatiba. Watachoweza kupata ni jeraha litalotoka usaha kwa miaka na miaka.


Dalili tunaziona kwani hakuna la maana lililopatikana hadi sasa tangu Bunge hilo lilipoanza vikao vyake vya kuipitia Rasimu ya Pili ya Katiba. Sababu sote tunaijua: ni kuingiliwa kisiasa kwa mchakato huo au labda tuseme kuingiliwa na vyama vya siasa, na hususan, na CCM.


Uingiliaji huo ulifikia kilele katika hotuba aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete alipolifungua rasmi Bunge hilo. Hotuba hiyo imetafsiriwa na wengi kuwa ilikuwa ni ya kuwatisha wananchi.


Kwa hakika, sheria inayouongoza mchakato wa Katiba mpya haijavipa vyama vya siasa jukumu lolote katika utungaji wa hiyo Katiba. Kwa hivyo inashangaza kuiona CCM ikijitwika kazi isiyo yake ya kuwa na usemi wa mwisho kuhusu nini kiwemo na nini kisiwemo katika Katiba mpya.


Kwa mujibu wa sheria uamuzi wa mwisho utakatwa na wananchi kwenye kura ya maoni. Na hivyo ndivyo inavyopasa iwe kama kweli watawala wetu ni waumini wa demokrasia.


Tulipoanza kuukumbatia mfumo huo wa kidemokrasia tulikuwa na shaka shaka kuhusu watawala wetu. Juu ya hivyo, tukijidanganya kwamba labda baada ya muda watabadilika na kuwa waumini wa dhati wa demokrasia kwani licha ya mapungufu ya mfumo huo wengi wakiamini na wangali wanaamini kwamba mfumo huo ni bora kushinda ule uliokuwa ukitutawala tangu uhuru wa Tanganyika, Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano.


Mfumo huo wa miaka ya 1960 hadi 1992 ulikuwa wa chama kimoja cha siasa. Kwa kawaida mfumo wa aina hiyo baadaye hugeuka na huwa mfumo wa udikteta. Huanzia kuwa udikteta wa wachache katika hicho chama kimoja kinachohalalishwa, halafu huishia kuwa mfumo wa udikteta wa mtu mmoja.


Tatizo kubwa lililoikabili Tanzania ilipokuwa inabadili njia na kuanza kuifuata demokrasia ya vyama vingi ni ukaidi wa chama kinachotawala wa kutoukubali kwa dhati huo mfumo mpya. Chama hicho kilifanikiwa kuwafanya watu waamini kwamba kwa kuwapo vyama vingi Tanzania imegeuka na kuwa Taifa la kidemokrasia. Hicho kilikuwa ni kiini macho tu.


Kwa kweli, chama cha CCM kinatenda mambo kana kwamba ndicho pekee chenye haki ya kufanya maamuzi makuu yanayoihusu Tanzania.


Mwenendo wa chama hicho katika shughuli za Bunge la Katiba unayathibitisha hayo. Jinsi CCM ilivyohamanika na ilivyokamia kuvidhibiti vikao vya Bunge hilo na kuwadhibiti wajumbe wake ni ishara moja ya hayo.


Tena wakereketwa wa CCM katika Bunge hilo wana kiburi cha hali ya juu. Na ndicho kilichowafanya waonekane kama vile wameingia bungeni na shoka wakidhamiria kuipasua vipande vipande Rasimu ya Pili ya Katiba, hasa vifungu vyake vinavyowakirihisha vikiwa pamoja na vile vya pendekezo la kuwa na Muungano wa aina ya shirikisho.


Niwazi kwamba kwa muda sasa tangu walipoanza kujidai kuwa wanafuata mfumo wa kidemokrasia watawala wetu wametuchujukia na tumewatoa maanani. Na ubaya wa mambo ni kwamba ule mfumo mpya wa siasa nao umeingia hatarini na huenda usinusurike madhali watawala wetu na chama chao wataendelea na tabia yao ya kulifanya Taifa la Tanzania kuwa ni lao peke yao.


Hata hivyo, watakuwa wanajidanganya wakidhania kwamba wananchi watalala kwa mseto wanaowalisha, mseto wa vitisho, chuki na uzushi. Lazima wang’amue kwamba wananchi wa leo si wa jana. Wa leo wameamka na hawakubali wala hawatokubali kuburuzwa.


Wananchi wanaelewa kwamba kuhusu suala hili la Katiba kinyume na ilivyokuwa wakati wa Tume za Nyalali na Kisanga, safari hii Rais wa Tanzania hana usemi wa mwisho. Hiyo ni haki yao wao wenyewe wananchi watakayoitumia wakati wa kura ya maoni kuhusu Katiba itayopendekezwa.

Chanzo:Raia mwema


Mjumbe Jr

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top