Ombi la
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mchungaji Christopher la kutaka Bunge hilo
livunjwe, limekuwa zito kwa Mwenyekiti Samuel Sitta.
Kutokana
na ugumu huo, Sitta amelazimika kumpatia barua Mtikila ili awasilishe
hoja yake kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye kisheria ana mamlaka hayo ya
kuvunja Bunge la Katiba, ambalo limekuwa likionekana kwenda mrama.
Mtikila,
ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Kidemokrasia na mjumbe wa Bunge la
Katiba aliwasilisha barua yenye hoja binafsi akitaka bunge hilo livunjwe
na wajumbe warejee makwao kwa madai kuwa chombo hicho cha kutunga
Katiba mpya hakijali maslahi ya umma na uongozi umekuwa haumtendei haki.
Majibu ya
barua hiyo yalikuwa hivi: "Nimeagizwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu
nikujulishe kwamba Bunge Maalumu halina uwezo wala mamlaka ya
kujitangaza kwamba ni haramu na hivyo livunjwe ; na kwamba hoja hiyo
haistahili kuwa hoja ya Bunge Maalumu," inasomeka barua hiyo
iliyoandikwa na katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad.
Akizungumza
na Mwananchi jana, Sitta alikiri kumpatia barua hiyo Mtikila ili aende
kwa Rais Kikwete kwa sababu hoja yake kutaka kuvunjwa Bunge haiwezi
kusikilizwa na chombo hicho kwa kuwa mwenye madaraka ya kuvunja Bunge ni
Rais pekee.
"Ni kweli
ametuletea hoja ya kuvunja Bunge. Ameandika mambo mengi, akitumia lugha
ya uchochezi, kama kudai kwamba 'Tanganyika imekuwa koloni la Zanzibar
kwa muda mrefu', lugha ya namna hii hatuwezi kuikubali," alisema Sitta.
Sitta alisema siyo kila kitu ambacho mjumbe anasema, ni lazima kifuatwe katika mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya.
"Mtu akija anasema anataka Bunge livunjwe amfuate aliyetuteua, siyo sisi wenyewe kujivunja," alisema Sitta.
Alisema
hoja ya Mtikila, ambaye alitishia kufungua kesi ya kuzuia Bunge la
Katiba kufanya kazi, ya kutaka Bunge kuvunjwa imekwenda kinyume kabisa
na taratibu za Bunge.
"Hoja hii
imekwenda nyuzi 180 kwa sababu aliyetuteua alitaka sisi tutunge katiba
kutokana na rasimu, ili sisi tupeleke kwa wananchi rasimu
iliyopendekezwa," alisema.
Mchungaji
Mtikila alikiri kupokea barua kutoka Ofisi ya Bunge ikimweleza jambo
moja; apeleke hoja yake kwa Rais Kikwete aliyeteua Bunge la Katiba.
Hata
hivyo, alisema hakusudii kwenda kumuona Rais Kikwete baada ya kushauriwa
kupitia barua ya Bunge kutokana na kutoa hoja ya kutaka kuvunjwa kwa
bunge hilo.
"Sitakwenda
kumuona Kikwete, bali ninajua kwamba tukishindwa kuipata Tanganyika
kwenye Bunge hili nitakwenda mahakama za kimataifa," alisema Mtikila
ambaye amekuwa akihubiri Utanganyika tangu nchi ilipoingia kwenye siasa
za vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya tisini.
Alisema
kwa sasa anasubiri kumaliza majadiliano juu ya sura ya kwanza na ya sita
ya rasimu ya katiba kuona mwelekeo na suala la muundo wa Muungano kuwa
wa serikali tatu litakwamishwa, ataondoka Dodoma na kurejea Dar es
Salaam kuandaa kesi.
Hoja
kubwa katika mchakato wa kutunga Katiba mpya iko kwenye muundo wa
Muungano baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwasilisha rasimu
inayoonyesha kuwa wengine wanataka muundo wa Muungano wa serikali tatu,
jambo ambalo linaonekana kupingwa na wajumbe kutoka chama tawala cha
CCM.
Bunge
hilo linaundwa na wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano,
wawakilishi wa Baraza la wawakilishi wa Zanzibar na wawakilishi wa
makundi mbalimbali wapatao 201 ambao walitangazwa na Rais Kikwete.
Lakini Mchungaji Mtikila anapingana na muundo wa Bunge la Katiba.
"Nitakwenda
mahakamani kupinga sheria yote ya Mabadiliko ya Katiba kwani waliopaswa
kushiriki Bunge la Katiba ni wajumbe waliochaguliwa na wananchi kwa
ajili ya Bunge la Katiba, na siyo hawa wabunge na wengine wa kuteuliwa,"
alisema.
Hoja ya Mtikila
Pamoja na
mambo mengine katika hoja yake, Mtikila analalamika kuwa amezuiwa
kuchangia katika Bunge hilo baada ya kuandikiwa barua na Ofisi ya Bunge.
Hata hivyo, katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Khamis Hamad alisema: "Hili kwangu ni jipya na sidhani kuwa linawezekana."
Mtikila
alisisitiza kuwa alipewa barua hiyo Jumatano iliyopita ikiwa ni majibu
ya barua yake aliyoiandika kwa ofisi hiyo wiki iliyopita.
"Nilianza
kuhisi baada ya kuona ninanyimwa kuchangia; nikaandika barua kuomba
maelezo kwa nini ninakosa nafasi ya kuchangia bungeni," alisema na
kuongeza:
"Lakini
juzi nilipokea barua kutoka kwa katibu wa Bunge ikinikataza kuchangia
tena bungeni kutokana na kauli zangu za kukosoa mchakato."
Alisema
kuwa alipomuuliza katibu sababu za uamuzi za kukatazwa kuchangia,
alijibiwa kuwa ni maagizo kutoka kwa mwenyekiti wa Bunge la Katiba,
Samuel Sitta.
"Hii imeniathiri sana mimi. Bunge hili limepotoka kwa kuwa wanachoangalia ni maslahi yao na si ya nchi," alisema.
Alisema
mchakato wote umekosewa kwa kuwaweka wabunge na wawakilishi kuwa sehemu
ya Bunge badala ya wananchi kuchagua wajumbe wa Bunge.
"Hakuna
nchi yoyote ambayo imefanya hivyo. Wanaharibu mabilioni ya fedha ambayo
hayataleta Katiba yenye uhalali wowote," alisema.
Alisema
endapo Sitta atashindwa kutatua jambo hilo, anakusudia kuunganisha
katika ushahidi wake kwenye kesi inayopinga mchakato wa Katiba.
Chanzo:Mwananchi
Post a Comment