Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema wanasiasa wanaomtuhumu
kwa kumsaliti Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuhusu Muungano,
ndiyo wasaliti kwa kuwa waliingiza kwenye Katiba, mambo yanayokinzana na
makubaliano ya Muungano huo.
Jaji Warioba amesema usaliti huo ni
pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuondoa mamlaka ya Bunge la
Muungano katika utungaji wa sheria, kuitambua Zanzibar kuwa nchi
inayojitegemea na kuongeza mambo ya Muungano bila kufuata Katiba.
Ametoa kauli hiyo kujibu mwendelezo wa
lugha za kejeli na matusi anazorushiwa na baadhi ya wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba wengi kutoka CCM na baadhi ya viongozi wa Serikali
baada ya Tume aliyoiongoza kupendekeza muundo wa serikali tatu.
Akizungumza juzi usiku katika kipindi
cha Dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, Jaji
Warioba alisema viongozi wa pande mbili za Muungano wanaomtuhumu, ndiyo
waliouvuruga Muungano huo
“Mwalimu aliacha Bunge likiwa na mamlaka
kamili, aliacha nchi ni moja, aliacha mambo ya Muungano 11 sasa
yamekuwa ni 22, kwa bahati nzuri Rais Jakaya Kikwete alieleza bungeni
hilo kwamba mambo hayo yaliongezekaje,” alisema na kuongeza:
“Katika kubaini kuongezeka kwa mambo ya
Muungano ndivyo ilikuwa inapunguza mamlaka kwa Zanzibar, mambo 11
yaliyoachwa na mwalimu yaliingizwa kikatiba lakini haya yaliyoongezeka
yalipatikana kienyeji.”
Jaji Warioba alisema enzi za uhai wake,
Mwalimu Nyerere aliheshimu na kuilinda Katiba hivyo, walioivunja ndiyo
wasaliti wa Muungano.
“Sasa kati ya mimi na wao ni nani
msaliti kwa Mwalimu, angekuwapo (Mwalimu) ni yupi angeonekana msaliti wa
Serikali ya Muungano? Wao ndiyo wameuvuruga, alichokiacha Mwalimu ni
tofauti na kinachoonekana kwa sasa,” alisema Jaji Warioba.
Kuhusu Bunge
Jaji Warioba alisema mipango mingi ya maendeleo inayopangwa ndani ya Bunge la Muungano inatekelezwa upande wa Bara pekee.
“Si hivyo tu, Bunge hilo linajadili
mambo ya Bara tu na halihusishi upande wa Zanzibar. Zanzibar nayo
inajadili mambo yake na kujiamulia lakini jina la Bunge hilo ni
Muungano,” alisema Jaji Warioba.
Kutokana na mazingira hayo, Jaji Warioba
alisema Zanzibar iliamua kuondoa mamlaka ya Bunge hilo katika utungaji
wa sheria kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema
sheria zinazotungwa katika Bunge hilo zitatumika ndani ya pande zote za
Muungano, lakini Zanzibar wakabadilisha hilo kupitia Katiba yao wakasema
sheria zote zitakazotungwa ndani ya Bunge hilo, lazima zipitiwe tena na
Baraza la Wawakilishi,” na kuongeza: “(Zanzibar) Hawakuishia hapo,
wakafanya mabadiliko ya Katiba mwaka 2010 iliyovunja Katiba ikiitambua
Zanzibar kama nchi kamili, ikaondoa mamlaka ya Rais wa Jamhuri kugawa
wilaya na mikoa kwa Zanzibar tofauti na Katiba ya Muungano, kwa maana
hiyo Zanzibar ikavunja nguvu ya Bunge la Muungano.”
Aidha, alisema hatua hiyo ilionekana
kuuvunja Muungano kwa vitendo baada ya kuvunja mamlaka ya Rais na
kutambua marais kamili katika nchi mbili tofauti.
“Kwa kawaida nchi inakuwa na amri jeshi
mkuu mmoja ambaye anapigiwa mizinga 21, Jeshi la Muungano linapiga
mizinga kwa marais wawili kitu ambacho hakiwezekani,” alisema.
Malalamiko ya Watanganyika
Jaji Warioba alisema Kwa upande wa
Tanzania Bara, walibaini malalamiko ya Watanganyika kuwa ni pamoja na
kukosa fursa mbalimbali ndani ya Zanzibar. “Watu wa bara nao wanasema
Zanzibar inashiriki Bunge la Muungano, inakagua miradi ya bara na
kuihoji lakini wao hawana nguvu ya kushiriki mambo hayo kwa upande wa
Zanzibar,” alisema.
Aliongeza: “Mbaya zaidi wanasema
Wazanzibari wanaweza kumiliki ardhi na kupata uraia kwa upande wa bara
lakini haki hizo haziwezi kupatikana kwa Mtanganyika, njia pekee tukaona
ni vyema Zanzibar nayo ilete mambo yake ndani ya Muungano lakini
ikashindikana.”
Hoja ya takwimu
Jaji Warioba aliwataka wajumbe wa Bunge
wasihangaike na takwimu badala yake wajibu maswali yaliyojitokeza kutoka
kwa washirika wa Muungano.
“Takwimu siyo tatizo, sisi hatukufanya
jambo jipya, ila ilikuwa ni kama marudio tu ya Tume ya Nyalali, wanahoji
takwimu hizo je, hawakuona dosari kwa takwimu za maoni ya asilimia 20
kwa jaji Nyalali?
Alisema Tume yake ilizunguka nchi nzima
ikiwa na waandishi waliorekodi kwa tepu, video na maandishi kwa ajili ya
kuweka kumbukumbu katika mtandao wa Tume.
MJUMBE Sr
WASALITI WA MWALIMU WALIOTAJWA NA WARIOBA HAWA HAPA1
Title: WASALITI WA MWALIMU WALIOTAJWA NA WARIOBA HAWA HAPA1
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema wanasiasa wanaomtuhumu kwa kumsaliti Baba wa Taifa, M...

Post a Comment