Meatu. WAFUASI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)wilayani Meatu mkoani Simiyu juzi waliwashambulia kwa mawe Wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakifanya maandalizi ya Mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Meatu,Meshack Opulukwa(CHADEMA) katika uwanja wa Stendi mjini Mwanhuzi. Tukio hilo lililotokea majira ya saa 5:30 asubuhi lilizua taharuki na hivyo kusababisha shughuli mbalimbali zilizokuwa zikifanyika katika eneo hilo na eneo la soko la Mwanhuzi kusimama kwa muda wa dakika 30 hadi hapo polisi walipofika na tuliza vurugu hizo. Watu walioshuhudia tukio hilo waliwaeleza waandishi wa habari kuwa wafuasi wa CHADEMA walikuwa wakipamba jukwaa la kuhutubia lililokuwa katika uwanja huo ambalo ni mali ya Halmashauri ya Wilaya. Mara walifika wafuasi wa CCM wapatao 20 na kuwataka wafuasi wa CHADEMA wasiende na kazi hiyo kwani hapo ni eneo ambalo diwani wa Kata ya Mwanhuzi mjini,Elia Shukia (CCM)analitumia kuonyeshea Runinga mashindano ya soka ya Kombe la Dunia. “Hilo eneo ambalo ndilo tunafanyia mikutano yote ya hadhara mjini Mwanhuzi kuna jukwaa ambalo ni mali ya Halmashauri wakati CHADEMA wakiendelea kulipamba walivamiwa na wafuasi wa CCM na kuwataka kuondoka mara moja kwani eneo hilo kwa sasa linamiikiwa na Diwani Shukia(CCM)na wenyewe wakagoma”Alisema John Ndago. Waliendelea kueleza kuwa baada ya mabishano yaliyochukua takribani dakika tano na kushindwa kuelewana ndipo wafuasi wa CCM walianza kuwashabulia wafuasi CHADEMA kwa kuwapiga kwa kutumia mawe,nondo na fimbo. Vurugu hizo ziliendelea kuwa kubwa baada ya wafuasi wa CHADEMA kujibu mapigo huku wakisaidiwa na baadhi ya wananchi kabla ya kutulizwa na Askari polisi kutoka kituo cha wilaya waliofika katika eneo hilo . Pamoja na Askari Polisi kutuliza vurugu hizo lakini ziliendelea ndipo askari wa kikosi cha kuzuia Ghasia (FFU)kutoka mkoa wa Simiyu walipowasili mjini humo na kuthibiti hali hiyo. Mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo wakiwa wanavuja damu sehemu mbalimbali za miili yao baada ya kupigwa na mawe. Inadaiwa vurugu hizo zilikuwa zimeandaliwa na baadhi ya viongozi wa CCM wilayani Meatu akiwemo diwani Diwani wa Kata ya Mwanhuzi,Elia Shukia kwa lengo la kuzuia mkutano huo usifanyike. Akizungumzia vurugu hizo Mlezi wa CHADEMA wilayani humo,Zacharia Maghembe alisema kuwa chama hicho kimesikitishwa na kitendo hicho cha wafuasi wa CCM kuwavamia wafuasi wao na kulitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua kali kwa wahusika vinginevyo sasa wamechoka kuvumilia vitendo hivyo. “Kitendo kilichofanywa na wenzetu wa CCM wa kuwavamia wafuasi wetu waliokuwa wakifanya maandalizi ya mkutano hakivumiliwi tunalitaka jeshi la polisi kuwakamata wote waliofanya vitendo hivyo kwani tunawafahamu kinyume cha hapo tumechoka kuonewa tutajibu mapigo”alisema Maghembe. Mbunge wa Jimbo la Meatu,Meshack Opulukwa alilaani tukio hilo na kusema hizo ni siasa za kihuni na za kizamani ambazo zinapaswa kulaaniwa na wapenda maendeleo wote na kudai kuwa viongozi wote wanaosimamia mipango hivyo hawataki kuongoza jamii. Polisi wilayani humo wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na vurugu hizo.
Post a Comment