Mbunge wa Chalinze (CCM),Ridhiwani Kikwete

Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete, amewashambulia wanahabari nchini kuwa asilimia kubwa ni makanjanja na kwamba wanapoandika habari wanasukumwa na weledi wa jinsi wanavyofikiria vichwani na itikadi zao za kisiasa.

Ridhiwani alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa mahafali ya wanafunzi ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika vyuo vikuu vya mjini Morogoro yaliyofanyika katika ukumbi wa bwalo la Umwema mjini humo.

“Asilimia kubwa ya waandishi tuliokuwa nao ni makanjanja, ni ukweli kabisa wanapokaa kwenye meza zao wanaandika vitu tu, wanapokaa kwenye ofisi zao wanaandika vitu tu, yaani mtu anapikapika tu vitu,” alisema.

Alisema siyo dhamira yake kuwasema vibaya wanahabari, lakini waandishi wengi hapa nchini wanasukumwa sana na weledi wa siasa zao jinsi wanavyofikiria vichwani mwao na itikadi ya siasa.

Aliongeza kuwa wakati mwingine hata jambo zuri likifanyika hawezi kulisifia badala yake kazi yake kubwa ni kuandika mambo ya ovyo ovyo tu.

“Mimi ningependa sana kuwasihi waandishi wetu hebu kidogo tuandike vitu vinavyofanana na hali halisi, hatusemi kuwa watu wanapofanya mabovu wanyamaziwe, hapana, wabovu waandikwe na mabovu yao, wanapofanya mazuri wasifiwe ili kuendelea kutiana moyo katika kulijenga taifa,” alisema.

Ridhiwani alisema Watanzania jambo kubwa wanalolihitaji ni amani na kwamba wasomi watambue kuwa nchi ipo mahali pazuri sana na amani inazidi kutawala tofauti na inavyoripotiwa na magazeti.

Alisema wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ya mwaka 2014/15, mambo yaliyofanywa na wizara hiyo katika kipindi cha 2013/2014 ni mazuri sana, lakini cha ajabu siku moja kabla ya kuanza kwa mjadala wa wizara hiyo, magazeti yaliandika Waziri Muhongo kikaangoni.

“Kikaango hicho kipi, haya ndiyo magazeti tuliyonayo, yanaandika andika tu yaani mpaka wakati mwingine nashindwa kuelewa,” alisema Ridhiwani.

Aliongeza kuwa wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kulizuka kelele kwa baadhi ya watu kwamba wanataka waandishi wawe huru, lakini yeye (Ridiwani) akawa anajiuliza moyoni hivi huo muswada wa habari ukipelekwa Bungeni hawatalia?

Wakati Ridhiwani akiwashambulia waandishi wa habari, amekuwa mwanasiasa kijana ambaye kila anakokwenda kwenye shughuli za kisiasa anafuatana na msururu wa waandishi ambao humpamba kwa habari nzuri.

Miongoni mwao, ni kikosi kikubwa cha waandishi alichokuwa nacho wakati wa kampeni za uchaguzi katika jimbo la Chalinze Aprili mwaka huu.

Katika harakati zake za kisiasa amekuwa akitumia waandishi wa habari kumpamba kwa nia ya kujijenga kisiasa kama ambavyo wamekuwa wakifanya wanasiasa wengi, wakiwamo ambao anawachukulia kama mfano wa kuigwa.

 Credit:Nipashe