
Sehemu ya Mji wa Morogoro
TUKIO la
mtoto Nasra Mvungi kuteswa kwa kufungiwa katika boksi ndani ya nyumba
kwa zaidi ya miaka mitatu na kufariki dunia baada ya kuokolewa na
wasamaria, limefanikisha kupatikana kwa mtoto mwingine mwenye matatizo
ya kiafya ambaye licha ya kuzaliwa miaka 18 iliyopita, inaelezwa
hajawahi kulia, kuongea, kukaa wala kutembea.
Mtoto
huyo mwenye mwonekano kama wa mtoto mwenye umri wa miaka mitano,
amepatikana baada ya wasamaria kutoa taarifa Dawati la Jinsia katika
Jeshi la Polisi wilayani hapa, wakiarifu kuwapo kwa mtoto mlemavu
anayenyanyaswa kama ilivyokuwa kwa mtoto Nasra `Mtoto wa Boksi’.
Katibu wa
Dawati la Jinsia, Koplo Janeth Maeda amethibitisha kuwapo kwa tukio
hilo, akisema walipokea taarifa za kuwapo kwa mtoto anayenyanyaswa,
hivyo kukimbilia eneo la tukio ili kumwokoa mtoto aliyedaiwa kuwapo
katika mateso ikiwa pamoja na kunyimwa huduma muhimu.
Hata
hivyo, anasema walichokishuhudia si mateso, bali ni hali duni ya
kimaisha ya wazazi wake, hivyo kulilazimu Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na Ustawi wa Jamii kumwokoa kwa kumkimbiza hospitali kwa
uchunguzi zaidi wa afya yake.
Anasema:
“Kwa kweli tulipopata taarifa hizo tulishtuka sana tukaamua kuwasha gari
na kuelekea eneo la Lukobe ambako ndiko tuliambiwa kuwa kuna mtoto huyo
na kumkuta mtoto huyo, lakini tofauti na tulivyoambiwa, tulimkuta akiwa
katika mazingira mazuri.
“Labda
kilichoonekana kwa wengine kama ni mateso ni kwa sababu wazazi wake
kutokuwa na uwezo wa kumudu matibabu tumeamua kusaidiana na ofisi ya
Ustawi wa Jamii Mkoa kumsaidia mtoto huyo kwa kuhakikisha anapatiwa
huduma ya matibabu anayostahili.”
Kwa
mujibu wa wazazi wa mtoto huyo wa kike aitwaye Farida, baba Abdallah
Kipingu na mkewe, Mwajuma Abdallah, wakazi wa Lukobe katika Manispaa ya
Morogoro, binti yao huyo alizaliwa mwaka 1996 na kwamba tangu azaliwe
hajawahi kulia.
Mama wa
mtoto, Mwajuma akiwa sambamba na mumewe alisema walimzaa Farida huko
Muheza mkoani Tanga na kwamba walimzalia nyumbani, lakini kutokana na
kushindwa kulia, wiki moja baadaye walikwenda Hospitali ya Wilaya ya
Muheza ili kujua kilichomsibu mtoto wao.
“Hatukupata
msaada, tukaendelea kumlea alipofikisha miezi minne ambao mara nyingi
ni muda wa kukaa, tulijaribisha kumkalisha, lakini hakukaa hivyo kwa
mara nyingine tukaenda hospitali, safari hii ya Mkoa wa Morogoro ambako
tumekuwa tunaishi, tukaambiwa mtoto ahudhurie mazoezi ya viungo.
“Tulihudhuria
mazoezi kwa muda mrefu hatukuona mabadiliko baadaye tukaamua kuhamia
kwenye kituo cha kulea watoto walemavu cha Amani Center, tukaambiwa
tuendelee ingawa hakukuwa na mabadiliko, tulipohamia Lukobe mwaka jana
hatukuweza tena kumpeleka kwenye mazoezi kutokana na kukosa uwezo wa
kifedha za kufanya mizunguko,” anasema.
Anasema
wamekuwa wakiendesha maisha kwa kutegemea biashara ya bidhaa ndogondogo
katika genge lao, msimamizi mkuu akiwa mumewe na kwamba yeye huhangaika
zaidi na mtoto.
“Hayo
ndiyo yamekuwa maisha yetu hadi kufikia wakati huu tulipopata msaada wa
Polisi na Ustawi wa Jamii,” anasema mama huyo aliyeiomba jamii kuwaombea
na kuwapa msaada wa hali na mali katika kufanikisha matibabu na malezi
ya binti yao ambaye kwa sasa amefikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa
Morogoro kwa uchunguzi zaidi.
Naye
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu aliwashukuru
wananchi kwa kuitikia mwito wa kutoa taarifa za matukio kama ya mtoto
Nasra, kwani imewafanya wafumbue macho na kutoa taarifa mbalimbali.
Alisema
taarifa zao zinaweza kuwa faraja kwa watoto na wazazi wengi wasiojua cha
kufanya baada ya kuelemewa na majukumu ya kutunza watoto wenye uhitaji
maalumu.
Hata
hivyo, aliitaka jamii kuwapeleka watoto wenye ulemavu na wenye matatizo
katika sehemu zinazohusika ili watoto hao waweze kupatiwa msaada na
hatimaye kuweza kuimarisha afya zao.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Mganga Mkuu Mfawidhi, Dk Rita Lyamuya
alisema baada ya kupata taarifa hizo taratibu za kumfanyia uchunguzi
zinaendelea ikiwa ni pamoja na kumpatia virutubisho
Na:Martha Magessa
MJUMBE Sr
Post a Comment