Unknown Unknown Author
Title: PICHA NA MAELEZO:MAAMBUKIZI VVU KITAIFA WANAWAKE 6.2% NA 3.8 WANAUME;JIJINI DAR YAPUNGUA! BAADHI YA SABABU ZA MAAMBUKIZI ZATAJWA HAPA!
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Terezia Mmbando (kulia) akitoa taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na Ukimwi katika jiji ...

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Terezia Mmbando (kulia) akitoa taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na Ukimwi katika jiji la Dar es salaam kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho alipotembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo kuangalia hatua zilizofikiwa katika kupambana na ugonjwa huo katika ziara yake ya siku nne.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw. Raymond Mushi akitoa tathmini ya hali ya maambukizi ya VVU katika jiji la Dar es salaam na hatua zinazochuliwa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kukabiliana na janga hilo mara baada ya kupokea ugeni kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi.
Meya wa Manispaa ya Ilala Mh. Jerry Silaa ambaye pia ni diwani wa kata ya Gongolamboto akitoa ufafanuzi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho  kwa kuhusu hatua iliyofikiwa na mikakati ya manispaa ya Ilala katika kukabiliana na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.
Meya wa Manispaa ya Ilala Mh. Jerry Silaa akifurahia jambo na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho (kulia) na Diwani wa Viti maalum Ilala Mh.Batuli Mziya (katikati) wakati wa ziara ya viongozi wa TACAIDS kata ya Gongolamboto.
Mmoja wa wanachama wa Asasi ya Vijana ya St. Camilus inayojihusisha na utoaji wa elimu kuhusu VVU na Ukimwi kwa vijana kupitia sanaa mbalimbali Bi. Aquila Mawenya akisoma taarifa ya utendaji kazi wa asasi hiyo kwa  Mwenyekiti wa wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Dkt. Fatma Mrisho alipokutana na wanachama wa Asasi hiyo Kiwalani jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho (katikati) akiwa na baadhi ya wanachama Asasi ya Vijana ya St. Camilus inayojihusisha na utoaji wa elimu kuhusu VVU na Ukimwi kwa vijana kupitia sanaa mbalimbali alipowatembela eneo la Kiwalani jijini Dar es salaam.
Baadhi ya viongozi wa manispaa ya Ilala wakiongozwa na Meya wa Manispaa hiyo Mh. Jerry Silaa (katikati) wakiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Dkt. Fatma Mrisho (wa tatu kutoka kulia) alipotembelea Kata ya Gongolamboto kuangalia hatua zilizofikiwa katika kupambana na ugonjwa huo katika ngazi ya kata.
Picha na 10. Mwenyekiti wa wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho akikutana na vijana wa kata ya Vingunguti wa Asasi ya Watoto na Vijana –CAFLO. Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho  akizungumza na viongozi na wakazi wa kata ya Gongolamboto jijini Dar es salaam alipotembelea eneo hilo kuangalia hatua zilizofikiwa katika kupambana na ugonjwa huo katika ngazi ya kata.
Katibu wa mtandao wa Vikoba vya watu wanaoishi na VVU (IDINEPA VICOBA) kata ya Kiwalani Bw. Shaban Mwasa Wamikole akimkabidhi risala ya kikundi hicho  Mwenyekiti wa wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Dkt. Fatma Mrisho alipokutana na wanachama wa kikundi hicho katika kata ya Kiwalani jijini Dar es salaam.
==== =======
MAAMBUKIZI YA VVU JIJINI DAR ES SALAAM YAPUNGUA.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
18/6/2014. Dar es salaam.

Licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za udhibiti wa maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, Jiji la Dar es salaam limefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 9.8 za mwaka 2007/2008 hadi kufikia asilimia 6.9 kutokana na jitihada zilizofanywa na serikali zikiwemo za uundaji wa kamati shirikishi za mkoa kudhibiti maambukizi hayo. 

Hayo yamebainishwa  katika taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na Ukimwi iliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Terezia Mmbando kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho alipotembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo kuangalia hatua zilizofikiwa katika kupambana na ugonjwa huo.

Akisoma taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam Bi. Mmbando ameeleza kuwa janga la Ukimwi ni tatizo la dunia nzima na limekuwa kikwazo cha maendeleo ya jamii hapa nchini na kuongeza kuwa jitihada za kudhibiti maambukizi ya Ukimwi jijini Dar es salaam zimechukuliwa kupunguza maambukizi ikiwa ni pamoja na uanzishaji rasmi wa kamati za kuratibu na kusimamia shughuli za kudhibiti Ukimwi kuanzia ngazi ya mkoa, halmashauri, ngazi ya kata na mtaa.

Amesema jiji la Dar es salaam linakabiliwa na changamoto ya ongezeko la kubwa la watu ikilinganishwa na mikoa  mingine hali inayochangia mwingiliano wa tamaduni, shughulim mbalimbali, masuala ya kijamii,kimila na kiuchumi na kuongeza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2012 idadi ya watu imefikia  4,364,54, wanaume wakiwa 2,125,786 na wanawake 2,238,755 sawa na ongezeko la asilimia 5 kwa mwaka.

Hali ya VVU na Ukimwi mkoa wa Dar es salaam.
Hali ya maambukizi ya Ukimwi katika jiji la Dar es salaam kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuhusu viashiria vya Ukimwi na Malaria mwaka 2011/2012 inaonesha kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kitaifa ni wastani wa asilimia 5.1 ambapo maambukizi kwa wanawake ni asilimia 6.2 na wanaume ni asilimia 3.8.

Sababu za maambukizi.
Miongoni mwa sababu zinazochangia kuendelea kuwepo kwa maambukizi mapya ya VVU katika mkoa wa Dar es salaam ni pamoja na kasi ya ukuaji wa jiji na shughuli za kibiashara hali inayosababisha mwingiliano wa watu na mahusiano ya kimapenzi pia baadhi ya wakazi kutobadili tabia licha ya kupatiwa elimu ya kujikinga na maambukizi ya ya ugonjwa huo.

Sababu nyingine ni hali ngumu ya uchumi hususani maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa wakazi wa kipato cha chini,kuongezeka kwa vitendo vya ngono isiyo salama hususani maeneo yenye nyumba nyingi za kulala wageni, kumbi za starehe, madangulo na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi ya madereva wa magari ya masafa marefu.

Aidha, ngoma za usiku zinazokesha  hasa maeneo ya pembezoni mwa jiji zinazoambatana na unywaji wa pombe kupita kiasi  na uwepo wa makundi maalum ya watu wanaofanya biashara ya ngono na wale wanaotumia dawa za kulevya hali inayowafanya washindwe kutoa maamuzi sahihi ya kujikinga na VVU ni miongoni mwa sababu zinazochangia maambukizi mapya ya VVU.

Hatua zilizochukuliwa kudhibiti maambukizi.
Mkoa kwa kushirikiana na halmashauri za manispaa na wadau mbalimbali pamoja na mambo mengine umeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU,kuhamasisha upimaji wa hiari wa VVU pia kuongeza nguvu katika mapambano ya kuzuia maabukizi kutoka mama kwenda kwa mtoto kupitia kliniki za afya ya uzazi. 

Hatua nyingine ni utoaji wa huduma za tiba na virutubisho kwa wagonjwa, kuwahudumia watoto yatima na wale wanaoishi mazingira hatarishi pia kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuhamasisha uundaji wa vikundi vya ujasiriamali kwa wanaoishi na VVU ili waweze kumudu gharama za maisha na uundaji wa vikundi vya sanaa vya vijana kwa ajili ya kutoa elimu ya VVU na Ukimwi kwa vijana walio katika mazingira hatarishi ya maambukizi katika jiji la Dar es salam.
Asante Blog za Mkoa

MJUMBE sr

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top