
Na Hudugu Ng'amilo
Bajeti ya
Sh50 bilioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya safari za Rais Jakaya
Kikwete katika mwaka ujao wa fedha ni miongoni mwa mafungu ya fedha
'yaliyopigwa panga' ili kuwezesha kupatikana kwa fedha za kugharimia
miradi ya maendeleo.
Habari
kutoka ndani ya kikao cha majadiliano baina ya Serikali na Kamati ya
Bunge ya Bajeti zinasema, Sh11 bilioni zimepunguzwa katika fungu hilo na
kubakiza Sh39 bilioni.
Hata
hivyo, kiasi kilichobakishwa ni ongezeko la asilimia 260 la Sh15 bilioni
zilizopitishwa na Bunge mwaka jana kwa ajili ya safari za Rais katika
mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30 mwaka huu.
"Katika
bajeti ya 2013/14 safari za Rais zilitengewa Sh15 bilioni lakini
inaonekana fedha zilizotumika ni nyingi zaidi maana ndani ya miezi
miwili tu zote zilikuwa zimemalizika," kilisema chanzo chetu na
kuongeza:
"Kwa hiyo
kwa mwaka 2014/15 Serikali ilimtengea Rais Sh50 bilioni za safari, ila
tumekata Sh11bilioni ili kupelekwa katika shughuli nyingine za
maendeleo. Kwa hiyo kwa mwaka ujao wa fedha, safari za Rais zitatengewa
Sh39 bilioni".
Awali,
ilielezwa kuwapo kwa mvutano mkali baina ya Serikali na Kamati ya Bunge
ya Bajeti, lakini jana mchana pande hizo zilikubaliana kukata asilimia
7.5 ya fedha katika baadhi ya mafungu ya matumizi mengineyo (OC) kutoka
katika wizara zote ili kuwezesha kupatikana kwa Sh230 bilioni ambazo
zinahitajika kwa ajili ya maendeleo hasa katika sekta tatu; afya,
miundombinu na kilimo.
"Bado
kikao kinaendelea na tangu asubuhi tumekata fedha katika fungu la
matumizi mengineyo, mfano chai katika ofisi za wizara pamoja na ununuzi
wa magazeti, ununuzi wa magari ya kifahari, mafuta, viburudisho, semina
na makongamano pamoja na safari za ndani," kilieleza chanzo chetu.
Chanzo
kingine kutoka Serikalini kilisema: "Katika siku ambazo tumevutana
kwenye kikao cha kamati ni leo (jana), lakini mwishoni tulifikia mwafaka
wa kukata kati ya asilimia saba na nane ya fedha za matumizi mengineyo
katika wizara zote, ili kupata fedha za maendeleo."
Juzi,
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema wizara yake inakusudia
kupitia bajeti za wizara zote ili kuhamisha fedha kutoka katika matumizi
yasiyo ya lazima ili zielekezwe katika mahitaji muhimu.
"Kama
wananchi wanakula mlo mmoja kwa siku, waliopo wizarani hawawezi kufa kwa
kukosa chai asubuhi. Tutafanya hivyo ili fedha hizo zipelekwe katika
shughuli za maendeleo.
Kesho
(jana) katika kikao cha mashauriano tutakwenda kuweka msimamo wa pamoja
katika jambo hilo. Wizara zisielekeze macho Wizara ya Fedha pekee, nazo
zinatakiwa kuwa na mikakati ya kubana matumizi yake."
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge alipoulizwa kuhusu hatua
iliyofikiwa katika majadiliano alisema: "Subirini itakaposomwa bajeti
mtajua kilichoamuliwa."Vyanzo vya mapato
Licha ya
kuwapo kwa makubaliano kuhusu suala la matumizi, vyanzo vya mapato
vimeendelea kuwa siri hata kwa wajumbe wa Kamati ya Bajeti.
Usiri wa
vyanzo hivyo ni moja ya mambo ambayo yalizua mvutano kutokana na wabunge
kutaka kufahamu ni kwa vipi Serikali itamudu kupata kiasi cha Sh19
trilioni kugharimia Bajeti ya 2014/15, wakati imeshindwa kutimiza
malengo ya kukusanya Sh18.2 trilioni kwa mwaka huu wa fedha.
Mmoja wa
wajumbe wa Kamati ya bajeti, Hamad Rashid Mohamed alisema Serikali
imekuwa ikishindwa kukusanya mapato ya kutosha kutokana na kung'ang'ania
kutekeleza miradi ambayo ingeweza kufanywa na sekta binafsi.
Mbunge
huyo wa Wawi (CUF), alitoa mfano wa miradi mikubwa ya kujenga reli,
bandari na barabara kwamba inaweza kutekelezwa na sekta binafsi kwa ubia
na Serikali.
Alisema
kutokana na mahitaji makubwa ya kifedha, Serikali imekuwa ikikisia
makusanyo makubwa ambayo haiwezi kufikia malengo yake, hivyo kuathiri
miradi mingi ya maendeleo.
"Sisi
tumekuwa tukiwaambia kama fedha za ziada zinapatikana, Bunge lipo walete
supplementy budget (Bajeti ya nyongeza) kuliko huu utaratibu wa sasa wa
kupitisha bajeti ya mapesa mengi ambayo hatuna uwezo wa kuyapata,"
alisema.
Alisema
tatizo lingine ni kukosekana kwa nidhamu ya ukusanyaji na matumizi ya
fedha... "Kuna miradi hewa na mingine fedha zinaonekana kwenda lakini
haijatekelezwa, haya ni mambo ambayo yanaifanya bajeti yetu
kutotekelezeka."
Jana,
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema Serikali itatangaza vyanzo
vyake vipya wakati wa kusoma bajeti yake bungeni... "Huo ndiyo utaratibu
wa kawaida kabisa miaka yote."
Akizungumzia
suala hilo, Nchemba alisema: "Hatuwezi kuweka wazi vyanzo vya mapato
hivi sasa, kwa sababu tulichonacho ni mapendekezo tu."
Alisema
mapendekezo hayo yatapelekwa Baraza la Mawaziri ambalo litaongozwa na
Rais Jakaya Kikwete ambaye anatarajiwa kuwasili Dodoma leo.
Post a Comment