WANANCHI WAANDAMANA NA KUFUNGA BARABARA!
WANANCHI wanaoishi Mivinjeni Kurasini katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam wameandamana na kufunga barabara ya Kilwa kwa muda wa zaidi ya masaa Matatu, wakiwa na mabango yenye ujumbe wa malalamiko ya kudai kulipwa fidia zao ili kupisha mradi wa ujenzi wa bandari kavu kwenye eneo hilo. Mashuhuda wa tukio hilo amesema kuwa wamefikia uamuzi huo kwa lengo la kuitaka Serikali kuwalipa fidia ya fedha za nyumba zao zilizowekewa alama na serikali kwa ajili ya kubomolewa na kupisha mradi wa ujenzi huo.
Shuhuda amesema vurugu hizo zimepelekea baadhi ya wananchi kujeruhiwa kwa kupigwa mabomu ya kutoa machozi pamoja na virungu, zoezi lililofanywa na Askari wa Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU).
Wakazi hao wamesema kuwa Serikali ilikubaliana na mwekezaji kuwalipa pesa zao na kutafutiwa viwanja huko Kibada lakini cha kusikitisha zoezi la ulipaji hundi lilisitishwa hapo jana mpaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka atakapotoa tamko lini walipwe.
Aidha, katika tukio hilo baadhi ya magari yaliyokuwa yanatumia barabara hiyo yalizuiwa kupita na wananchi hao kwa kuweka mawe barabarani na matairi ya magari wakitaka kuyachoma kwa lengo la kuzuia shughuli zozote kutoendelea katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa ITV, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik akiongea kwa njia ya simu amemuagiza Mkuu wa Wilaya kuhakikisha watu hao wanatawanywa na yeyote atakayekaidi achukuliwe hatua za kisheria kwani si taratibu sahihi kufunga barabara na kusababisha usumbufu kwa watumiaji barabara ambao hawahusiki.
Chanzo;Fikra Pevu
Post a Comment