Unknown Unknown Author
Title: TAFAKARI NA MJENGWA:ASILI YA NENO DALADALA......! NA HATIMA YA UCHUMI WETU KAMA TAIFA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Je, Unaijua Historia Ya ' Daladala'? Ndugu zangu, Asili ya neno Daladala ni jina tulilolitohoa kutoka sarafu ya Marekani, ya...
Je, Unaijua Historia Ya ' Daladala'?
Ndugu zangu,
Asili ya neno Daladala ni jina tulilolitohoa kutoka sarafu ya Marekani, yaani, Dola. Nakumbuka kwenye miaka ya 80 mwanzoni , na katikati ya shida kubwa ya usafiri Dar, nauli za usafiri wa vibasi vidogo vidogo ikaongezeka na kufikia shilingi tano kwa safari moja. Ndipo hapo tuliweza kumsikia kondakta akiita; " Kariakoo Dala ..dala..dala... dala!"
Maana, shilingi tano yetu iliyokuwa nzito kidogo hata kuishika na yenye pembe sita ilikuwa na thamani sawa na dola moja ya Marekani. Ndipo hapo, shilingi tano yetu ikabatizwa jina la ' Dala'.
Kuna mengi ya kutafakari kuhusiana na uchumi na jamii yetu. Tujiulize; wakati wasafiri wa daladala enzi hizo walikuwa ni watu wa kipato cha chini na hata cha kati, je , wasafiri wa daladala wa leo ni watu wa aina gani? Wasafiri wa Mabasi ya Mwendo Kasi ni watu wa aina gani?
Je, anayepanda daladala leo, na anayepanda mabasi ya mwendo kasi anatazamwa vipi? Ni mtu asiye na uwezo kifedha au anaweza kuwa ni mtu anayeona kuliacha gari lake nyumbani na kupanda dala dala amefanya mawili; amebana matumizi na kuelekeza fedha zake kwingine na hata kutunza mazingira. Maana, magari mengi mijini yanachafua mazingira.
Je, ni kwa nini uchumi wetu wakati huo ulikuwa na nguvu kutuwezesha kubatiza sarafu zetu kwa fedha za kigeni kama dala kwa shilingi tano. Wengine waliita gwala.
Tuliweza pia kuibatiza noti ya shilingi 20 kwa kuiita ' Paundi' ikiwa na maana, thamani ya paundi moja ya Uingereza wakati huo ilikuwa ni sawa na shilingi 20 za Tanzania. Ni kwenye miaka ya 80.
Je, rasilimali zetu ikiwamo gesi na mafuta vinaweza kuturudisha kwenda kuwa ' Taifa Kubwa' kama tulivyokuwa wakati fulani. Maana, nakumbuka nikiwa mdogo nilisikia redioni taarifa ya habari ikisema kuwa ' Tanzania imetoa msaada wa magunia ( Sikumbuki idadi) ya kunde na maharage kwa nchi ya India kutokana na mafuriko yaliyowakumba. Nilisikia pia Tanzania ikitoa msaada wa chakula kwa nchi ya Msumbiji na kwingineko zilizokumbwa na maafa.
Je, tunaweza kurudia kuwa ' Taifa Kubwa' kiuchumi kama tutaendelea kuruhusu karibu kila nchi kubwa kiuchumi kuwa na benki zao hapa kwetu? Maana siku hizi hapa kwetu kuna benki za Wahindi mpaka Wapakistani! Je, na sisi tuna mabenki kwao?
Na tafsiri ya benki hizo si ina maana pia kuwa nchi hizo zimeamua kujenga ' Vihenge' vyao kwetu kuhifadhia wanavyovuna hapa kwetu na kusafirisha kwenda kula kwao.
Na tuendelee kujadili daladala na uchumi wetu...! Na cha kukuhakikishia, ni kuwa hakuna hatari ya miaka michache ijayo, Daladala zikabatizwa jina jipya, kuitwa 'Bukubuku!' Kwa maana ya nauli za Daladala zitapanda kufikia shilingi elfu moja kwa safari. Jina ' Daladala' litabaki daima kuwa na maana ya usafiri wa ndani wa njia fupi fupi.
Picha hiyo juu niliilipiga mwaka 1988 pale Posta ya Zamani. Huo ulikuwa ni usafiri tulioutumia enzi hizo, maarufu kama ' Chai- Maharage'. Ni moja ya picha zangu za zamani sana zilizo kwenye Maktaba yangu.

Maggid.

Imepakuliwa Mjengwa blog

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top