Kuwasilishwa kwa Rasimu hiyo jana kulitokana na
kupatikana kwa maridhiano juzi usiku kati ya uongozi wa Bunge na
viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unaovishirikisha vyama
vya upinzani na wajumbe wanaotokana na makundi yaliyotajwa katika
kifungu cha 22(1)(C) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83.
Umoja huo ulianzishwa kwa lengo la kuhakikisha mchakato wa Katiba
unaiwezesha nchi yetu kupata Katiba Mpya na iliyo bora.
Ni vigumu kuelezea ukubwa wa vurugu zilizotokea
bungeni juzi kutokana na ufinyu wa nafasi katika safu hii. Hata hivyo,
viongozi wa Ukawa walitangaza mapema juzi kwamba wangepinga, pamoja na
mambo mengine, ukiukwaji wa Kanuni na wangezuia ratiba kuendelea hadi
kwanza yasikilizwe madai yao ya kumtaka Rais Kikwete afungue Bunge kabla
ya kuwasilishwa kwa Rasimu ya Katiba.Ndiyo maana Jaji Warioba
aliposimama kwenye mimbari ya Bunge tayari kuwasilisha Rasimu hiyo,
baadhi ya wajumbe walipiga kelele na kugonga meza, hivyo kumfanya
ashindwe kufanya kazi hiyo. Kama tulivyodokeza hapo juu, uwasilishaji
huo ulifanyika jana baada ya maridhiano kupatikana.
Sisi hatuwezi kuunga mkono vurugu Bungeni lakini
tunadhani kwamba tukio hilo litakuwa limetoa fundisho kwa Mwenyekiti wa
Bunge kwamba kamwe hataweza kuongoza chombo hicho pasipo kufuata Kanuni
zilizotungwa kuendesha shughuli zake.
Mwenyekiti huyo anapaswa kujua kwamba alivunja
Kanuni ya 7(1)(g) na (h) ambazo zimeweka mpangilio wa shughuli zote za
Bunge la Katiba. Ratiba hiyo ilionyesha wazi kwamba hotuba ya ufunguzi
ambayo itatolewa na Rais, itatangulia na kufuatiwa na uwasilishaji wa
Rasimu ya Katiba.
Tunashawishika kusema ukiukwaji huo wa Kanuni
ulifanywa kwa makusudi, hasa tukizingatia uzoefu alioupata akiwa Spika
wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano. Yatakuwa makosa makubwa iwapo
atadhani kwamba makundi yenye wajumbe wachache yatakubali kuburuzwa,
kwani Bunge la Katiba ni tofauti na Bunge la kawaida ambalo limekuwa na
dhana potofu kwamba kundi lenye wabunge wengi ndilo lina haki ya
kusikilizwa. Tunakubaliana na viongozi wa Ukawa wanapohadharisha kwamba
Katiba hii itatumiwa na vizazi na vizazi, hivyo ni lazima itengenezwe
kwa misingi ya kujali utu wa kila mtu, kuheshimiana na kukubaliana.
Ubabe na kukiuka Kanuni kwa kisingizio cha ‘busara
za Mwenyekiti’ havikubaliki, isipokuwa tu pale Kanuni zinapokuwa
hazielekezi chochote.
Tukio kubwa lililokuwa likisubiriwa ni
uwasilishwaji wa Rasimu ya Katiba ambao ulifanywa jana na Jaji Warioba
kwa utulivu, umakini, busara na ustadi mkubwa.
Alipewa muda wa kutosha kutoa ufafanuzi wa masuala
mazito na alifanya hivyo bila ya kuwaburuza. Wajumbe sasa wanayo Rasimu
mbele yao ambayo watapaswa kuijadili bila ya jazba, bali kwa kuzingatia
hoja badala ya kuangalia nani anatoa hoja.
Ni matumaini yetu kwamba wajumbe wataweka mbele masilahi ya taifa badala ya misimamo na itikadi za kisiasa.
Mjumbe Jr
Post a Comment