Hivi sasa Tanzania ipo katika mchakato wa kuandaa Katiba Mpya, hii ni nafasi ya kipekee kabisa ya kutengeneza taifa jipya. Katiba hii ndiyo ngao itakayowalinda Watanzania kwa zaidi ya miaka 50 ijayo.
Rasimu ya Katiba iliyoanza kupitiwa na wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba imetajwa makundi mengi sana lakini imeacha wasanii ambao ni sehemu kubwa ya jamii, wao wanachukua robo ya Watanzania wote.
Wasanii wameamua kupaza sauti zao na kudai haki ambayo wameshindwa kuipata katika kipindi cha katiba ya mwanzo, huku wakisaidiwa na baadhi ya wanasiasa ili kuhakikisha mapendekezo yao kuhusu Katiba Mpya waliyowasilisha kwa Tume yanafanyiwa kazi.
Ombi kuu la wasanii ni kuhakikisha kazi ya sanaa inathaminiwa kama kazi, huku wakihitaji kazi zao, miliki bunifu kuthaminiwa na kulindwa.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba anasema kuna kila haja ya kurasimisha sanaa na kuitambua kama sekta rasmi.
“Maisha ya taifa na urithi wa taifa unahifadhiwa katika kazi za sanaa, iwe ni katika nyimbo, mashairi, michoro, riwaya au maigizo na kazi nyinginezo, kazi zinazotokana na vipaji na bidii za Watanzania. Taifa lisilotambua na kuthamini kazi za sanaa ni taifa lisilojitambua, tuanze kujitambua kwa kuwatambua wasanii na kuzilinda kazi zao kwenye Katiba hii mpya,” anasema January Makamba.
Mbali na mwanasiasa huyu, wabunge wengine Livingstone Lusinde (Mtera mkoani Dodoma) na Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), maarufu Sugu, pia wameungana na wasanii hawa katika kampeni hii muhimu.
Wasemavyo wasanii
Umoja wa wasanii wote nchini kupitia shirikisho la sanaa, unataka sanaa irasimishwe kwa maendeleo ya sasa na yajayo, IP (intellectual property right) miliki bunifu kwenye sanaa kwani ndiyo ngao yao, na isipowezekana leo haitawezekana mpaka miaka 50 ijayo.
Wasanii wengi wa rap na hiphop wanasema kuna haja ya Serikali kuangalia upya, kwani Tanzania ina zaidi ya wasanii milioni 10, lakini kilio chao kikubwa wameachwa na hawatambuliki katika Rasimu ya Katiba inayopitiwa bungeni Dodoma.
Mchizi Mox yeye anasema kutokuwekwa sheria ya kuitambua sanaa kama sekta rasmi ni kuukandamiza uchumi wa nchi.
Chanzo:Mwananchi leo
Mjumbe Jr
Post a Comment