Mtwara. Watu watatu mkoani Mtwara wamepoteza maisha kufuatia
kuzama kwa mtumbwi waliokuwa wakisafiria katika Bahari ya Hindi kutoka
Kitongoji cha Mwale kuja Mtwara Mjini kwa ajili ya shughuli zao za kila
siku.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara,
Zelothe Stephen aliyeongea na waandishi wa habari katika Hospitali ya
Rufaa ya Ligula akiwa ameongozana na uongozi wa mkoa, alisema ajali hiyo
ilitokea saa 5 asubuhi mita kama 100 kutoka eneo la ufukwe wa kienyeji
baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupatwa na misukosuko.
Zelothe alisema ajali hiyo imesababisha vifo
vitatu, majeruhi 21 wakiwemo watoto wadogo wawili kati ya mwaka mmoja na
kuwataka wananchi kuwa makini na vyombo wanavyotumia kusafiria
ikizingatiwa kwa sasa hali ya hewa siyo nzuri kutokna na mvua
zinazoendelea kunyesha.
Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Mwanahamis
Juma (31) na Habiba Masoud (13) wote wakazi wa Mwalena Rahma Abdul (25)
mkazi wa kitongoji cha Ngw’ale.
Naye Mkuu wa Mkoa, Kanali Mstaafu Joseph
Simbakalia alieleza kuwa ajali hiyo imesikitisha sana na kwamba kifo
hakina matarajio kwani waliokumbwa na mkasa huo walikuwa wakienda kwenye
shughuli zao za kila kujitafutia kipato.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Dk
Shaibu Maarifa alikiri kupokea majeruhi na maiti za ajali hiyo na kusema
kuwa wanawahudumia ipasavyo ili waweze kurudi katika hali zao za
kawaida.
Mmoja wa majeruhi walionusirika katika ajali hiyo,
Sophia Kassim (28) alimwambia mwandishi wa habari hizi wakati wa
mahojiano kuwa mtumbwi waliokuwa wakisafiria ulijaza watu kupita kiasi
na kwamba abria wote walikuwa wanawake isipokuwa dereva na msaidizi
wake.
Chanzo:Mwananchi
Na Mjumbe Jr
Chanzo:Mwananchi
Na Mjumbe Jr
Post a Comment