Jumuiya
ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), maarufu kama
Uamsho imemjia juu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), William Lukuvi, ikimtaka athibitishe kauli yake ya
kuwahusisha na Chama cha Wananchi (CUF) pamoja na vitendo vya uhalifu
visiwani humo.
Uhalifu
ambao Lukuvi anadaiwa kuihusisha Uamsho ndani ya Bunge Maalumu la Katiba
na kanisani, ni pamoja na kuuawa kwa padri, kuchoma makanisa na
uharibifu wa miundombinu Zanzibar.
Kutokana
na hali hiyo, Uamsho wamemwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo,
Samuel Sitta, kumtaka ambane Lukuvi athibitishe tuhuma hizo, vinginevyo
watatumia sheria kumchukulia hatua.
Nakala ya
barua hiyo, ambayo imeambatanishwa na nakala ya DVD inayoonyesha kauli
zinazodaiwa kuwa ni za uchochezi wa kidini uliofanywa na Lukuvi,
imepelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete; Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed
Shein; Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Spika wa Baraza la Wawakilishi na
wawakilishi wote.
Nakala ya
barua hiyo pia imepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Amiri wa
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Amiri wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Zanzibar, Ofisi ya Mufti Zanzibar, Jumuiya ya Maimamu Zanzibar
(Jumaza), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Maimamu wote.
Pia
imepelekwa kwa Waziri wa Mipango, Sera na Uratibu wa Bunge, Ofisi ya
Spika wa Bunge, Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Kamati ya
Maridhiano Zanzibar, vyombo vya habari, Waislamu na wapenda amani wote
Tanzania.
Naibu
Katibu Mkuu wa Uamsho, Sheikh Yusuph Hamis Yusuph, alitangaza tamko la
jumuiya hiyo, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam
jana.
Alisema
wanapeleka nakala za DVD hiyo kwa Sitta ili awaonyeshe wajumbe wa Bunge
hilo jinsi zinavyoonyesha uchochezi wa kidini uliofanywa na Lukuvi ndani
ya kanisa na bungeni.
Pia jumuiya hiyo inadai kuwa Lukuvi amekuwa ikidai sera za Uamsho ni sera za chama cha CUF na pia wanapenda sana kufanya vurugu.
Alisema
wamelazimika kufunga safari kutoka Zanzibari kwenda Dar es Salaam
kuzungumza na waandishi wa habari kutokana na kuchoshwa na maneno,
ambayo yamekuwa yakitolewa na Lukuvi katika Bunge hilo dhidi ya Uamsho.
"Lukuvi
alitakiwa kuzungumzia jinsi katiba mpya itakavyopatikana na siyo
kuzungumzia maneno ambayo hana ushahidi nayo juu ya Uamsho," alisema
Sheikh Yusuph.
Alisema
kutokana na kitendo cha Lukuvi kuuzungumza maneno machafu na ya
uchochezi dhidi ya Uamsho bungeni, wanamuomba Sitta atumie nafasi
aliyonayo amwamuru atoe ushahidi wowote anaoujua juu ya jumuiya hiyo.
Sheikh Yusuph alisema kama Lukuvi atashindwa kufanya hivyo, watawasiliana na wanasheria na hatua dhidi yake zitafuatwa.
Alisema
pia wanataka kujua kauli ya serikali juu ya kauli ya Lukuvi aliyoitoa
katika Kanisa la Methodist Jimbo la Dodoma kuwa iwapo serikali tatu
zitakuwapo nchi itachukuliwa na wanajeshi, pia makanisa yote nchini
yatafungwa na nchi itakosa amani.
Lukuvi alitoa kauli hiyo katika kanisa hilo wakati wa sherehe za kumtawaza Mchungaji Joseph Bundala kuwa askofu.
Sheikh
Yusuph pia alisema Lukuvi hakuishia hapo, bali alienda mbali zaidi kwa
kudai kuwa wanaotaka nchi yao Wazanzibari hawawezi kujitegemea, bali
wanataka serikali ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa nchi ya Kiislamu
na kwamba, Uamsho ni taasisi ya Waislamu wenye msimamo mkali.
"Sisi
Jumuiya tuna amini hayo ni maoni ya serikali kwa vile yeye amekwenda kwa
niaba ya waziri mkuu. Pia ni msemaji wa wizara na mpaka sasa serikali
kwa nini imekaa kimya na hiyo inaonyesha kwamba, inaunga mkono ubaguzi
wa dini aliouchochea Lukuvu," alisema.
Alisema
mwaka 2004 Jumuiya hiyo ilituhumiwa kuhusika na vurugu zilizotokea
Zanzibar, ikiwamo milipuko ya mabomu, kuchomwa makanisa, kuchomwa gari
la polisi na kuharibiwa kwa miundombinu.
Sheikh
Yusuph alisema kwa matukio hayo, ziliundwa tume mbili kwa ajili ya
uchunguzi, lakini mpaka sasa ni miaka 10, matokeo ya uchunguzi huo bado
hayajatolewa.
Alisema
Uamsho inasikitishwa sana pale viongozi wa dini ya Kiislamu
wanapozungumza masuala ya kijamii na kisiasa wanaonekana wametekeleza
katiba na uhuru wao wa kujieleza.
Lakini
akasema kwa bahati mbaya inapotokea kwa viongozi wa Kiislamu kutoa maoni
yao juu ya mambo hayo, hutokea baadhi ya viongozi wa serikali kuwalaumu
na kuwatuhumu juu ya uvunjifu wa amani, uchochezi, kuchanganya dini na
siasa na kutaka kusababisha vurugu.
Alisema Watanzania wanatakiwa kujionea Lukuvi alivyokwenda kuchanganya dini na siasa kanisani.
Sheikh
Yusuph alisema kibaya zaidi Lukuvi alileta uchochezi kati ya Waislamu na
Wakristo na kutangaza wazi dhamira ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar kuwa ni uadui na kuukandamiza Uislamu na Waislamu.
Alisema
Uamisho ni taasisi iliyosajiliwa kihalali na SMZ na kwamba, tangu
ilipopata usajili, imekuwa ikifanya kazi zake kisheria na haijawahi
kupatikana na hatia ya aina yoyote ya uvunjifu wa sheria.
Sheikh
Yusuph alisema mbali na hayo, hata viongozi wa Uamsho hawajawahi
kupatikana na hatia zaidi ya kufunguliwa kesi, ambazo hadi
hazijathibitishwa.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment