Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba amesema baadhi ya wajumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba wametumia vibaya Bunge hilo kwa kumshambulia
na kumsingizia mambo ya uongo kwa makusudi, akisema matusi yanayotolewa
dhidi yake yanamuumiza.
Aidha,
Warioba amesema ingawa haelewi kwa nini wanaomshambulia wameamua kutumia
lugha za matusi dhidi yake binafsi, hatajutia kuchaguliwa kuiongoza
tume hiyo kwa kuwa ilikusudia kuwaletea maendeleo wananchi wote kwa
kuwapatia Katiba wanayoitaka.
Kauli
hiyo ya Jaji Warioba imekuja wakati baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu
la Katiba na viongozi wa CCM wakiikosoa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba
kwa maneno makali,huku wakimshutumu na kumkejeli yeye na baadhi ya
wajumbe wa tume aliyoiongoza.
Akizungumza
kwa mifano katika mahojiano na gazeti hili jana, Warioba alisema kuwa
anawashashangaa wajumbe hao na viongozi wa CCM kwa kuacha kuijadili
Rasimu ya Katiba, badala yake wanamkosoa yeye na kumsingizia maneno
yasiyo ya kweli.
"Bulembo
(Abdallah Bulembo mjumbe wa Bunge na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa
CCM) amenitukana, amenitukana... amesema niliwahi kupokea rushwa huku
akijua kabisa kuwa ni uongo. Yeye ni kiongozi wa Kamati Kuu ya CCM,
anasema uongo akijua ni uongo. Kwanza mimi simjui wala sijawahi kumwona
huyu mtu naambiwa tu anatoka Mara," alisema Jaji Warioba kwa sauti ya
upole iliyoashiria kuumizwa.
Aliongeza
kwamba siyo mara ya kwanza kwa Bulembo kumshambulia kwa lugha za
matusi, kwani aliwahi kufanya hivyo tena kwenye moja ya mikutano ya CCM
mkoani Tanga.
"Alifanya hivyo Tanga, anachokifanya siyo kitu cha mzaha kwa sababu anafahamu kilichotokea," alisema.
Akizungumzia
kauli aliyoitoa Waziri Hawa Ghasia wakati akichangia mjadala wa Rasimu
ya Mabadiliko ya Katiba aliyemtaka Jaji Warioba kufunga mdomo kutokana
na kazi yake ya kuwasilisha Rasimu kumalizika, Jaji Warioba alisema:
"Wao wanataka waseme uongo, mtu mwingine asiseme kitu."
Warioba
alieleza kuwa tangu lugha za matusi na kejeli zilipoanza kutolewa dhidi
yake, baadhi ya watu walimshauri kwenda mahakamani kufungua kesi, lakini
alikataa kwa kile alichodai kuliheshimu Bunge.
Alisema
Bunge ndiyo lenye mamlaka ya kufuatilia na kudhibiti kauli zinazotolewa
bungeni, kama wahusika hawafanyi hivyo hawezi kuchukua hatua yoyote.
"Kama
kinga ya Bunge inatumika vibaya unafikiri mimi nitafanya nini? Sina nia
ya kuchukua hatua, watu walipendekeza niende mahakamani, kuna wanasheria
walisema hata nisipokwenda, wao watakwenda mahakamani nikawazuia,"
alisema Warioba ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu.
Akisimulia
kuhusu uchaguzi wa ubunge wa mwaka 1995 ambapo aligombea na kutuhumiwa
kupokea rushwa na kufungiwa kwa miaka minne, Warioba alisema taarifa
hizo siyo sahihi kwa kuwa aliyepokea rushwa ni aliyekuwa mgombea kwa
tiketi ya NCCR Mageuzi (wakati huo), Stephen Wassira ambaye sasa yuko
CCM na ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu."Uchaguzi
ule ulikuwa umejaa sana rushwa, tukaenda mahakamani, Wassira akafungiwa
asigombee," alisema.
Akizungumzia
maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar, Warioba alisema: "Mimi ni muumini wa muungano, kwa miaka 50
taifa limekaa kwa amani, mshikamano na umoja. Ni kweli tumekuwa na
matatizo lakini yanaweza kutafutiwa ufumbuzi.
CHANZO MWANANCHI
CHANZO MWANANCHI
MJUMBE Sr.
Post a Comment