Serikali imepandisha maradufu ada kwa wanafunzi wanaosomea ualimu kwenye vyuo vya ualimu nchini kuanzia muhula ujao wa masomo.
Ada hizo kwa wale wa ngazi za cheti na stashahada ambazo
zimeongezwa kwa karibu mara mbili au zaidi ya zile zilizokuwa zikilipwa
awali. Uamuzi huo ambao huenda ukawaathiri zaidi wanafunzi ambao waliona
ualimu kama kimbilio, unaelezwa na baadhi ya wadau wakiwamo walimu,
wanafunzi na hata wakufunzi wa baadhi ya vyuo nchini kuwa ni wa ghafla.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakufunzi, uamuzi huo umetolewa
kupitia waraka wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na unatarajiwa
kuanza kutekelezwa muhula wa pili wa masomo utakaoanza Julai 2, mwaka
huu.
Kabla ya kupandishwa kwa ada hizo, wanafunzi wanaosomea
ualimu kwa ngazi ya cheti walikuwa wakilipa Sh200,000, lakini sasa
watalazimika kulipa Sh300,000, ikiwa ni ongezeko la asilimia 50.
Kwa wale wanaochukua stashahada watalazimika kulipa Sh400,000
kwa masomo ya Sanaa na Sh600,000 kwa masomo ya Sayansi kutoka Sh200,
000 za awali.
Mhasibu wa Chuo cha Ualimu cha Mtwara, aliyekataa kutaja jina
lake kwa kuwa siyo msemaji wa chuo hicho, alithibitisha kupokea waraka
wa Serikali unaowataka kupandisha ada, lakini alisisitiza kuwa Mkuu wa
Chuo ndiye angeweza kufafanua zaidi kuhusu ongezeko hilo.
“Taarifa hizo ni za kweli ada imepanda, kama umezipata kutoka
wizarani hivyo ndivyo ilivyo kwa hiyo huna sababu ya kupata taarifa
zaidi kutoka kwetu,” alisema mhasibu huyo.
Awali, habari zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa
Serikali imefikia uamuzi huo kutokana na uhaba wa fedha na ugumu wa
kuviendesha vyuo hivyo.
Habari zinasema kwa muda mrefu sasa, Serikali imekuwa
ikidaiwa na wazabuni fedha nyingi, jambo ambalo limeathiri pia
uendeshaji wa vyuo vikiwamo vya ualimu.
Baadhi ya wakufunzi wameeleza kuwa fedha za ada sehemu yake
itatumika kutatua matatizo ya uhaba wa fedha ambao umekuwa ukiwakabili
na hivyo kuathiri utoaji wa huduma zikiwamo za vyakula.
Wizara ya Elimu
Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi
Bunyazu alisema viwango vilivyoongezwa siyo vikubwa ikilinganishwa na
hali ya ugumu wa maisha ilivyo sasa nchini.
“Unamweka mtu mwaka mzima anakula, analala, anasoma…kweli
unaona hiyo ada hiyo ni kubwa? Bado siyo kubwa kiasi cha kushtua watu,”
alisema Bunyazu.
Aidha, Bunyazu alisema kuwa wanafunzi watakaopata daraja la
kwanza katika masomo ya Sayansi na Hisabati na kuingia katika vyuo vya
ualimu vya Serikali watasomeshwa bure na wale watakaopata daraja la pili
na la tatu watapewa mkopo.
Wengine wazungumza
Meneja wa Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Shirika la
HakiElimu, Godfrey Boniventura akizungumzia suala hilo jana, alisema
kuwa siyo kweli kwamba serikali haina fedha za kutosha ndiyo maana
inaongeza ada, ila inadhani kuwa idadi ya walimu waliopo inatosha.
“Serikali imeamua kupandisha ada kwa kudhani kuwa walimu
waliopo wanatosha, lakini ikumbuke kuwa kuna walimu wengi wazee
wanaostaafu kila mwaka, wengine hawaripoti shuleni, hivyo tunahitaji
kuwa na benki ya walimu,” alisema Boniventura.
MWANANCHI
Post a Comment