Unknown Unknown Author
Title: KAMERA ZA CCTV KUFUNGWA MITAANI Z'BAR!
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
MAENEO mbalimbali visiwani Zanzibar, yamepangwa kuwekwa kamera za CCTV, ...


KAMERA ZA CCTV KUFUNGWA MITAANI Z’BAR


Zanzibari_f5ac2.jpg
MAENEO mbalimbali visiwani Zanzibar, yamepangwa kuwekwa kamera za CCTV, kukabili matukio ya uhalifu. Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk amesema mchakato wa utafiti wa kuweka kamera hizo, umekamilika na kipaumbele ni eneo la Mji Mkongwe.
Mbarouk alisema hayo wakati akijibu hoja mbalimbali za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, waliochangia makadirio mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/2015 katika Baraza Wawakilishi.
Alisema kampuni mbili, zilipewa kazi hiyo ya kuweka kamera za CCTV katika maeneo mbalimbali , ambapo kipaumbele ni Mji Mkongwe wa Zanzibar.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni hizo tayari zimewasilisha taarifa yake serikalini kwa ajili ya uchambuzi wa kina na ripoti yake itatangazwa kwa wananchi,” alisema.
Alisema uwekaji wa kamera za CCTV ni muhimu kwa ajili ya kukabili matukio ya uhalifu vitendo vya uhalifu ambavyo huathiri maisha ya watu na maendeleo ya sekta ya utalii.
Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alitaka kufahamu mikakati ya kuweka kamera za CCTV za kurekodi matukio mbalimbali , ikiwemo ya uhalifu katika eneo la Mji Mkongwe. Jussa alisema kama mradi huo wa kuweka kamera ungekamilika na kufanya kazi, matukio mengi ikiwemo kumwagiwa tindikali kwa raia wawili wanawake kutoka Uingereza, kungedhibitiwa na wahusika wangekamatwa.
Awali, Mbarouk alisisitiza suala la kuimarishwa kwa amani na utulivu nchini na alitaka jamii kuachana na vitendo vya uhalifu ambavyo ni tishio kwa maisha ya watu. Alisema matukio mbalimbali ikiwemo ya hivi karibuni la kulipuliwa bomu eneo la Darajani, kunatishia amani ya nchi pamoja na wageni kutembelea Zanzibar.
“Sekta ya utalii inategemea sana amani na utulivu na ikivurugika tu, basi hakuna mgeni atakayezuru Zanzibar katika mazingira ya vurugu na fujo,” alisema.
Uvaaji baibui Wakati huo huo, Mwakilishi wa Viti Maalumu, Asha Bakari Makame, alisema kutokana na kuwepo matukio ya ugaidi, suala la watu kupekuliwa zaidi, hususani wanawake waliovaa baibui ni jambo la kawaida.
Alisema yapo matukio ya wanawake, kutumia vibaya mavazi hayo, kutokana na wengine kuficha sura zao kwa lengo la kufanya uhalifu huo. “Mimi sipingi matumizi ya kivazi cha baibui…lakini kufuatia kuibuka kwa matukio ya uhalifu na vitendo vya ugaidi, wanawake waliovaa mabaibui wanalazimika kupekuliwa,” alisema.
Alisema mbinu za uhalifu zimeongezeka siku hizi hali ambayo pia wanaume wanaweza kutumia vazi hilo kwa ajili ya kutekeleza uhalifu. Vazi hilo ambalo ni maarufu kwa wakazi wa mwambao wa pwani ya Afrika ya Afrika, hususani Zanzibar, lilizua mjadala jana kwenye Baraza la Wawakilishi baada ya baadhi ya wajumbe wanawake, kulalamika kwamba wanaofanya kazi kwenye vyombo vya habari vya Serikali ya Zanzibar, wanalazimishwa kuvua mavazi hayo wanapoingia kazini.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo, Bihindi Khamis Hamadi alisema uvaaji baibui kwa wanawake, wanapokuwa kazini ni upendeleo na si utaratibu wa kazi.
Alisema utaratibu wa kazi na masharti yake, upo wazi kwamba vazi hilo haliruhusiwi kuvaliwa sehemu ya kazi.
“Mheshimiwa Naibu Spika yapo malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa Serikali kwamba wanazuiliwa kuvaa mabaibui katika sehemu ya kazi…ukweli unabakia kuwa, vazi la baibui kazini haliruhusiwi na kinachofanyika ni mazoea tu kwa wanawake hao,” alisema.
Alikiri pamoja kwamba ni sehemu ya utamaduni wa wananchi wa Zanzibar, wanawake wanapoingia kazini na mavazi hayo, hutakiwa kuyavua na kuyahifadhi katika sehemu maalumu hadi wanapoondoka kazini.
Serikali yazima ugaidi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana aliliambia Bunge mjini Dodoma kwamba matukio ya uhalifu yanayotokea Zanzibar, ikiwemo kumwagia viongozi tindikali na utumiaji wa mabomu ya kurusha kwa mkono, yalipangwa kuwa mengi zaidi, lakini Serikali imeyadhibiti. Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Betty Machangu (CCM).
Pinda alisema baada ya matukio hayo Zanzibar, Serikali ilijipanga vizuri ikiwemo kutumia vyombo vya kimataifa, kujua chanzo cha matukio hayo na katika harakati hizo, walibaini kulikuwa kutokee matukio mengi zaidi, Serikali ikayazuia.
Katika swali lake kwenye kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu, Machangu alitaka kauli ya Serikali kuhusu kuibuka kwa vikundi vya kihalifu vya vijana na vingine vyenye tabia ya kigaidi.
Alitaja baadhi ya vikundi hivyo ni Panya Road, Kiboko Msheli, Komando Yosso na Toto Tundu, na vingine vilivyotokea Mtwara ambavyo vilikuwa vikipewa mafunzo vichakani na kwamba yako madai, baadhi walipelekwa Somalia.
Machangu pia alitaka kufahamu kauli ya Serikali kuhusu matukio ya Zanzibar kuhusu mauaji ya padre na kumwagiwa tindikali kwa mashekhe.
Katika ufafanuzi wake, Pinda alisema Machangu amechanganya mambo mawili katika swali lake, moja la ugaidi na lingine la uhalifu wa kawaida.
Katika suala la uhalifu la vikundi hivyo kupora vitu na kukimbia, Polisi imeshafanyia kazi. “Pale Dar es Salaam hali sasa ni shwari. Naomba vijana wajiepushe na vitu vitakavyowakutanisha na mkono wa dola,” alisema.
Pinda ametoa kauli hiyo, wakati mwishoni mwa wiki iliyopita mtu mmoja alifariki dunia na wengine saba kujeruhiwa baada ya kurushiwa bomu na watu wasiojulikana katika eneo la Darajani, muda mfupi baada ya kuhudhuria mawaidha yaliyokuwa yakitolewa na Shekhe Kassim Mafuta Kassim (38) mkazi wa Pongwe mkoani Tanga.
Aliyefariki dunia kwa bomu hilo ni Muhammed Khatib Mkombalaguha. Tukio hilo la mlipuko ni la nne kutokea mwaka huu. Mengine ni yaliyotokea Kanisa la Evangelist lililopo maeneo ya Fuoni Machi 2, Kanisa la Anglikana, Mkunazini, Februari 24 na mlipuko mwingine ulitokea kwenye hoteli ya kitalii ya Mercury ilioko Forodhani. Vilevile, Zanzibar imeandamwa na matukio ya kumwagiwa watu tindikali pamoja na kushambuliwa kwa risasi.
Habari hii imeandikwa na Joseph Lugendo, Dodoma na Khatib Sulemain, Zanzibar.
CHANZO:HABARILEO

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top