KAMPUNI
ya ujenzi ya Strabag International GmbH inayojenga barabara ya Mradi wa
Mabasi yaendayo Haraka (DART) imetangaza mabadiliko ya muda katika eneo
la Ubungo jijini Dar es salaam kuanzia kesho na kesho kutwa usiku
kutokana na ujenzi unaoendelea wa barabara.
Akiongea
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano
wa kampuni hiyo, Bwana Yahya Mkumba, alisema kazi hiyo itahusu ujenzi
katika makutano ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Nelson Mandela
katika eneo la Ubungo.Alisema
ujenzi huo utakaoanza leo utasababisha kufungwa kwa baadhi ya njia
katika barabara hizo kuanzia saa nne usiku hadi saa 12 asubuhi kesho
Jumamosi.Akielezea
zaidi alisema katika awamu ya kwanza ujenzi huo utahusisha eneo la
upande wa kulia la makutano la barabara ya Sam Nujoma na Morogoro ambalo
litafungwa.
“Hali
hii itasababisha magari yanayotoka maeneo ya Buguruni na Tabata
kuelekea maeneo ya Mwenge kutoweza kutumia njia ya Sam Nujoma
watakapofika taa za Ubungo,” alisema.Alifafanua
kuwa magari hayo yatalazimika kufuata alama zitakazowaelekeza kupita
katika barabara za mradi zinazojengwa hadi barabara ya Shekilango ambapo
wataweza kukutana tena na Sam Nujoma kwa kutumia barabara ya Igesa.
Pia
magari yatakayokuwa yanatokea Sinza kupitia barabara ya Igesa
hayataweza kuelekea eneo la Ubungo yatakapofika katika makutano ya
barabara za Igesa na Sam Nujoma.
Alifafanua
kuwa magari yanayotumia barabara ya Morogoro kutokea maeneo ya Mbezi na
Kimara yatalazimika kuchepuka kulia na kutumia barabara za mabasi ya
mwendo wa haraka yatakapofika eneo la Kibo ambapo patakuwa na kizuizi.
Bw.
Mkumba alisema katika awamu ya pili ya ujenzi huo, eneo la upande wa
kushoto la makutano ya barabara za Morogoro na Nelson Mandela litafungwa
siku ya Jumamosi kuanzia saa nne usiku hadi saa 12 asubuhi siku ya
Jumapili.
Katika
awamu hii, alisema, watumia magari yatakayokuwa yanatokea eneo la
Mwenge kutumia barabara ya Sam Nujoma yatalazimika kuchepuka kushoto
kukamata barabara ya Igesa kisha Shekilango.
Pia
magari yatakayokuwa yanatokea barabara ya Nelson Mandela na kutaka
kuelekea mjini kwa kutumia njia ya Morogoro yatalazimika kuchepuka
kushoto na kwenda kugeukia eneo la Kibo ili kuikamata barabara ya
Morogoro.
“Tunaomba
radhi kwa usumbufu wowote utakaotokea,” alisema Bwana Mkumba na
kuongeza kuwa pamoja tunajenga na hivyo usumbufu utakuwa ni wa muda
mfupi.
Mradi wa Mabasi yaendayo haraka unatarajiwa kuondoa adha ya foleni katika jiji hilo na kuleta ufanisi wa usafiri.
Ubungo Tabata Diversion
Post a Comment