Sakata
la ukwapuaji wa pesa katika akaunti ya ESCROW, lachukua sura mpya,
wakati serikali ikesema fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo hazikuwa za
umma, wapo wanaodai kuwa fedha hizo zilikuwa za umma, mmoja wa wabunge
ambaye wako mstari wa mbele kulishikia bango sakata hilo Zitto Kabwe
ameamua kutoka hadharani na kulitolea ufafanuzi sakata hilo huku
akiwalaumu wapinzani kukaa kimya kulipigia kelele suala hilo na
kumuachia Kafulila, ingawa ushahidi unaonesha kuwa kambi ya upinzani
ulilipigia kelele suala hilo hadi kuamua kutoka nje na hata kwa maneno
yake mwenyewe Kafulila ndani ya Bunge alisema kuwa yeye na Mnyika
walipeleka ushahidi wa sakata hilo kwa Spika.
Yafuatayo ni maelezo ya Zitto Kabwe kuhusu sakata hilo alivyoandika katika ukurasa wake wa facebook.
Kwa mara nyingine serikali kupitia viongozi na watendaji wake akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba kiasi cha Dola za Marekani milioni 250 zilizopaswa kuendelea kuwapo katika ‘Tegeta Escrow Account’ si mali ya serikali na hivyo si mali ya umma. Akaunti hiyo ilifunguliwa na serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na kampuni ya Independent Power Limited (IPTL).
Kwa bahati mbaya sana viongozi wa serikali wamekuwa wakiendelea kurudia
kuueneza huo uongo kwamba fedha hizo si mali ya umma. Inasikitisha pia
kwamba vyombo vya habari vimekuwa navyo vikibeba na kusambaza huo uongo
bila kuhoji na kuchunguza. Inashangaza sana pia asasi za kiraia nazo
zimekaa kimya. Inatisha na kushangaa tena kuona wapinzani wakimwachia
suala hili Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, pekee
wakati mapambano dhidi ya rushwa ni ajenda kuu ya wapinzani. Kafulila
amekuwa akiendelea kuhoji suala hilo bungeni peke yake bila kupata
kuungwa mkono na kupewa msaada wa aina yoyote kutoka kwa wenzake wa
kambi ya upinzani bungeni.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilielekeza kuwapo kwa
ukaguzi maalumu kwenye akaunti hiyo ya Tegeta escrow account iliyokuwa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwa ndani yake kulikuwapo fedha za
umma. PAC haina sababu yoyote ya kufuatilia fedha za watu binafsi. Mwaka
2009 iliyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilitoa
maelekezo kwa BoT kutothubutu kutoa fedha hizo. Agizo hilo la POAC
lilitokana na sababu kwamba fedha hizo zilikuwa ndani ya hesabu za
Tanesco.
Akaunti ya ‘Tegeta escrow’ ilifunguliwa kutokana na kuwapo kutoelewana
kuhusiana na gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na
kuuzwa kwa TANESCO. Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID) katika
uamuzi wake wa Februari, 2014 ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco
walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL. Kwa
uamuzi huo ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadiwa kwenye
akaunti hiyo maalumu ya escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco
baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali.
Hesabu za mwaka wa fedha ulioishia Disemba 2012 za Tanesco zinaonyesha
wazi kwamba fedha hizo ni mali ya shirika hilo la umma linalomilikiwa na
serikali kwa asilimia mia moja. Fedha za kampuni ni suala la kisheria
kama inavyobainishwa katika sheria ya kampuni ya mwaka 2002.
Kwa maelezo hayo na hoja hizo, inakuaje serikali ianze kudai kwamba
fedha hizo si mali ya umma? Hivi inawezekanaje kwa fedha za mtu binafsi
zikaingizwa katika hesabu za shirika la umma linalomilikiwa na serikali
kwa asilimia 100? Ni lini fedha hizo zimekoma kuwa za umma? Je ni baada
ya baadhi ya watendaji wa serikali kula njama za kuzichukua fedha hizo
kwa kushirikiana na ‘mwekezaji’ aliyechafuka kwa ufisadi duniani?
Serikali inadanganya waziwazi kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma.
Umma una haki ya kukumbushwa kwamba madai hayo yalitolewa pia katika
lile sakata la ufisadi maarufu wa EPA unaofanana kwa kila hali na huu wa
sasa wa ‘Tegeta Escrow’.
Hoja nyingine ni kwamba, Mbunge Kafulila alisema kwamba Jaji Utamwa wa
Mahakama Kuu ya Tanzania hakutoa uamuzi wa kuchukuliwa fedha kutoka
akaunti ya ‘Tegeta Escrow’. Nimepitia kwa makini hukumu ya Jaji Utamwa
na kubaini kwamba hakuna popote alipotaja akaunti ya ‘Escrow’. Hata
hivyo, nilipopitia muhstasari wa kikao kati ya TANESCO, IPTL na Wizara
ya Nishati na Madini, ndipo kwa mara ya kwanza nikakuta wametafsiri
uamuzi wa mahakama wakidai kwamba fedha zote za ‘Tegeta Escrow’ zipewe
kampuni ya PAP (inamilikiwa kwa asilimia 50 na Harbinder Singh na 50% na
Simba Trust iliyosajiliwa Australia). Hiki ndicho kikao kilichofanya
maamuzi ya kuiba na kugawana wenyewe fedha hizo (Hukumu ya Jaji Utamwa
na muhstasari wa kikao vinaambatanishwa).
Wote waliohudhuria kikao hicho kilichojipa mamlaka ya kutafsiri hukumu
ya Mahakama Kuu, wanapaswa kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani kwa
mujibu wa sheria zilizopo. Inawezekana vipi uamuzi wa mahakama
ukatafsiriwa na kikao cha Wizara? Muhstasari wa kikao hicho ndio
uliowasilishwa Benki Kuu (BoT) kuhalalisha madai kwamba fedha hizo
lazima zitolewa kutoka akaunti ya Escrow.
Fedha zinazohusiana na akaunti ya Escrow ni Dola za Marekani milioni
250, katia ya hizo Dola milioni 122 zilizokuwa BoT zimeshatolewa na
kiasi kilichosalia Dola milioni 128 zitalipwa na Tanesco kutokana na
fedha zake kwa madai ya kushindwa kulipa kwa wakati. Fedha zilizolipwa
ni zile ambazo zimetoka Wizara ya Nishati na Madini ambayo kisheria ndio
walipaswa kulipia gharama za uzalishaji umeme (capacity charge) fedha
zilizotoka kwa walipa kodi.
Ikumbukwe kwamba uhamishaji wa asilimia 70 ya hisa za IPTL kwenda PAP
umeambatana na nyaraka za kughushi kutokana na kutokuwepo kabisa kwa
uthibitisho wa cheti halisi cha hisa (share certificate) kutoka kampuni
ya Mechmar kwenda kampuni ya Piperlink. Nyaraka za TRA zinaonyesha
kwamba hisa hizo (70%) ziliuzwa kwa Shilingi za Kitanzania milioni sita
(6) tu. Na bado hakuna ushahidi kuonyesha kwamba uhamishaji huo wa hisa
ulipata baraka za mamlaka husika kama inavyotakiwa na sheria za nchi.
Wakati huyo anayejiita mmiliki mpya wa IPTL aliposaini mkataba wa
kuchukua fedha kutoka akaunti ya Escrow zilizokuwapo BoT, hakuwa mmiliki
halali kisheria kwani kodi ililipwa siku moja baada ya wao kupokea
fedha kutoka BoT. Sheria inataka kutolewa kwa cheti na Kamishna wa TRA
kama uthibitisho kwamba kodi yote imelipwa ipasavyo (Sheria ya Fedha ya
2012 kifungu cha 29).
Ni nani wamiliki wengine wa kampuni ya PAP? Uchunguzi ni muhimu
ukawalenga vigogo na wanasiasa wakubwa wakiwamo watendaji waandamizi wa
Wizara ya Nishati na Madini.
Inapaswa tutafakari kuona kwamba Harbinder Singh aliyechukua fedha za
Escrow, anamiliki vitalu vya mafuta na gesi kupitia kampuni iitwayo
HydroTanz ambayo nayo imesajiliwa nchini Australia, ikiwa na anwani sawa
na ya kampuni ya Simba Trust. Kitalu hicho cha mafuta kinaitwa ‘Mnazi
Bay North’, jirani kabisa na ugunduzi mkubwa wa hivi karibuni mkoani
Mtwara.
Tunatarajia kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), atafichua
ukweli wa sakata hili na TAKUKURU itawafikisha mahakamani wahusika bila
kujali nyadhifa zao serikalini.
Kauli ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi,
kwamba kuna watu waliokula rushwa na kwamba nyaraka zinazotajwa ni
karatasi za kuuzia vitumbua, ni kauli zenye kuonyesha kutapatapa kwa
watendaji serikalini. Hakuna hata mahali pamoja ambapo nimemtaja mtu
kuwa ni mwizi zaidi ya kuwasilisha hoja zinazohitaji majibu mwafaka na
si matusi, vitisho na tuhuma za kuzusha. Nyaraka za TRA haziwezi kuwa za
kufungua maandazi kama ambavyo hukumu ya Jaji wa Mahakama Kuu haiwezi
kuwa karatasi za kufungia maandazi na badala yake ni nyaraka halali
zinazohitaji maelezo kutoka kwa viongozi na watendaji wa serikali badala
ya kuropoka na kuporomosha matusi.
Hali kadhalika, Bunge lina kila sababu kupitia sheria yake ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge kulinda hadhi yake kutoka kwa watendaji
kama Maswi ambao wanatoa matamshi ya kuonyesha kwamba chombo hicho ni
chombo cha watu wasiofaa na kwamba watu wanaofaa wanazungumza nje ya
Bunge. Maswi na wengine kama wana ushahidi wa rushwa dhidi ya mbunge ama
yeyote hawapaswi kupayuka ovyo bali kwa nafasi zao wanaweza kuwasiliana
na vyombo vya dola kama TAKUKURU na polisi ili wachunguze na kuchukua
hatua kama ambavyo vinawachunguza wao.
Kauli ya Maswi kwamba “wanaume” hawazungumzi ndani ya Bunge si tu
udhalilishaji wa chombo hicho bali pia inaashiria ugonjwa wa mfumo dume
uliotawala miongoni mwa viongozi wetu kwa maana kwamba wanaume ndio
wenye hadhi, uwezo na heshima na wanawake ni dhaifu na wasiostahili
heshima. Tufumbue macho tuone na tuondoe hisia binafsi zenye kubebwa na
itikadi, chuki na misimamo yetu ya kisiasa. Tuwe wazi.
MJUMBE Sr
Post a Comment