Unknown Unknown Author
Title: WALIMU KUUNDIWA TUME
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, ametangaza uamuzi wa Serikali wa kuunda Tume ya Elimu, itakayoshughulika na ajira na nidhamu y...

PindaBungeni_641cc.jpg
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, ametangaza uamuzi wa Serikali wa kuunda Tume ya Elimu, itakayoshughulika na ajira na nidhamu ya walimu, kukabili changamoto zinazowakabili walimu nchini.
Alitoa tangazo hilo jana bungeni mjini Dodoma, katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu (CCM).
“Sasa Serikali imekubali kuanzisha chombo maalumu, kitakachoshughulikia nidhamu na ajira za walimu, tunatarajia kinaweza kutusaidia,” alisema Pinda na kufafanua kuwa uanzishwaji wa chombo hicho umeshakubaliwa na Baraza la Mawaziri.
Dk Kafumu katika swali lake, alisema tatizo la malipo ya walimu ni la siku nyingi , akataka Pinda aseme lini suala la deni la walimu litaisha.
Kutokana na kuendelea kwa tatizo hilo, Dk Kafumu alisema wiki iliyopita walimu katika jimbo analotoka la Igunga, waliandamana mpaka ofisi ya Mkurugenzi wa Elimu (DED) na kumfungia ofisini, ingawa pamoja na hatua hizo, bado hawajalipwa madai yao.
Akifafanua, changamoto zinazowakabili walimu nchini, ambazo tume hiyo inatarajiwa kuja kutoa ufumbuzi wake, Pinda alisema tatizo kubwa linatokana na walimu kuhamia shule ambazo hawakupangiwa awali.
Pinda alisema changamoto zinazowakabili walimu zipo za aina mbili, moja madai ya posho zao na stahiki zingine na pili, tatizo la kukosa malipo mara wanapoanza kazi.
Alifafanua kuwa kinachochelewesha kupata malipo yao, ni tabia ya walimu kuhamia shule ambayo hawakupangiwa, na majina yao yanapoingizwa katika mfumo wa kielektroniki, mfumo huo unakataa kwa kuwa jina linakuwa katika shule ambayo hawakupangiwa.
Aliwataka walimu kuacha kuhama shule kienyeji, badala yake wafuate utaratibu kwa kuhama kihalali, ili mfumo huo wa kielektroniki, utambue uhamisho wao.
Kwa mujibu wa Pinda, kwa sasa kuna mfumo mwingine unaotumika, lakini pia huo mwalimu akihama kienyeji, itachukua muda kwa mfumo huo kumtambua.
Hatua ya Serikali kukubali kuundwa kwa tume ya elimu, kunatokana na baadhi ya wabunge, kuhimiza uundwaji wa Tume ya Kudumu ya Elimu, itakayochunguza mfumo wa elimu nchini.
Wabunge hao walipigia chapuo tume hiyo, wakati walipokuwa wakichangia hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha 2014/2015 iliyowasilishwa na waziri wake, Dk Shukuru Kawambwa.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR Mageuzi), alisema; “Tumwombe Rais aunde Tume ya Kudumu ya Elimu kwa sababu kwa hali inavyokwenda ni mbaya sana na napendekeza Tume hii ishughulike na kudhibiti mambo yote yanayofanya kutetereka kwa ubora elimu nchini”.
Chanzo;Habarileo

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top