Unknown Unknown Author
Title: WANAO DAIWA UDOM KUFANYA MITIHANI
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SERIKALI imewahakikishia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) walioshindwa kulipa ada kwamba watafanya mtihani na kam...

SERIKALI imewahakikishia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) walioshindwa kulipa ada kwamba watafanya mtihani na kama yapo madeni, watayalipa baada ya kumaliza.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitoa msimamo huo jana kutokana na swali la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) aliyesema zipo taarifa, wanafunzi 500 wa chuo hicho wamezuiwa kufanya mitihani yao kwa kushindwa kulipa ada za mitihani.
“Je, Serikali inachukua hatua gani kuwasaidia?” alihoji Mbunge huyo katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu. Pinda alisema Serikali itahakikisha wanafunzi hao, wanaruhusiwa kufanya mitihani yao na kama kuna madeni wanayodaiwa, watayalipa baada ya kumaliza mitihani hiyo.
Alisema yeye na serikali, watafuatilia kwa karibu kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi. “Ni imani yangu na sidhani kama tutaruhusu wanafunzi hao, washindwe kufanya mitihani kwa sababu ya suala la ada,” alisema.
Alisisitiza, hata kama baadhi yao, watakuwa wamelipa nusu ya ada, au wengine hawajalipa kabisa, watafanya tu mitihani hiyo.
“Haiwezekani mtu asome chuo kikuu miaka mitatu au minne, halafu anafika kwenye mitihani ya mwisho anazuiliwa kufanya mitihani. Tutalitafutia ufumbuzi wa haraka suala hili”, alisema.
Aidha alimshukuru mbunge kwa kumpa taarifa ambayo kwa mujibu wake, hakuwa nayo.
CHANZO:HABARILEO 

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top