Kijana Amosi Ng’arare Marale Sasi,(22)
anayesumbuliwa na uvimbe usoni.
Alikuja Muhimbili ili akafanyiwe upasuaji India,
alipelekwa akarudishwa bila kutibiwa, awaita
ndugu zake hospitalini.
Kijana Amosi Ng’arare Marale Sasi,(22) mkazi
wa Kijiji cha Kizaru, Kata ya Mryaza, wilayani
Musoma Vijijni amepoteza mwelekeo wa maisha
baada ya ndoto yake ya kusoma hadi chuo kikuu
kuishia njiani kutokana na matatizo ya ugonjwa
wa ajabu ambao unamtesa kwa kipindi cha
miaka 18.
MUHIMBILI MIAKA MITATU
Kijana huyo ambaye yupo Muhimbili kwa zaidi ya
miaka mitatu sasa alikuja katika hospitali hiyo
kwa lengo la kupatiwa matibabu tangu mwaka
2011, hata hivyo, baada ya uchunguzi
iligundulika kwamba matibabu yake ni mpaka
apelekwe nchini India.
INDIA AFIKA HAKUTIBIWA
Katika mahojiano na mwandishi wa habari hii
wiki iliyopita katika Jengo la Sewahaji, wodi
namba 23, Amosi akionekana mwenye uso wenye
huzuni alisema Oktoba 14, 2014 alipelekwa India
kwa matibabu lakini baada ya kufika huko
hakuna kilichofanyika.
“Nilipelekwa India katika Hospitali ya Apolo,
tulikaa kule mwezi mzima na ofisa moja wa
ustawi wa jamii kutoka hapa Muhimbili ambaye
alinipeleka lakini cha ajabu ni kwamba ilipofika
Novemba 19 mwaka jana, niliambiwa nijiandae
kwa kurudi nyumbani (Tanzania) kesho yake.
“Niliuliza kwa nini nirudishwe nyumbani wakati
sijatibiwa? Nikaambiwa kwamba ni uamuzi
uliofikiwa na taarifa zaidi nitajulishwa hapa
nyumbani.
Kijana Amosi Ng’arare Marale Sasi akiuguza
uvimbe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
ARUDISHWA MUHIMBILI
“Tulipanda ndege Novemba 20 mwaka jana na
kutua hapa Tanzania, nilirudishwa wodini
Muhimbili. Niliambiwa nisubiri siku nyingine
nitapelekwa tena huko India, nilishangaa nikaona
ningoje.
“Sasa ni muda mrefu sijajulishwa chochote
nimekua nikiishi hapa bila kujua hatima ya
maisha yangu, na bado najiuliza kwa nini
nipelekwe India halafu nirudishwe bila
matibabu?”alihoji Amosi huku akitokwa machozi.
HISTORIA YA UGONJWA
“Nilizaliwa nikiwa sina tatizo la aina yoyote
nikiwa na miaka minne baba akawa amefariki
dunia nikabaki na mama ambaye alikua akitulea
na ndugu zangu na kipato chake kinategemea
kilimo cha jembe la mkono.
“Nilipofikisha umri wa miaka mine ndipo
nilipoanza kupata tatizo hili kwa kutokwa na
kipele kilichokuwa kinawasha. Mama alinipeleka
hospitali mbalimbali kabla ya kupelekwa
Bugando na hapa Muhimbili,” alisema Amosi.
Msemaji wa Hospitali ya Muhimbili hakupatika
ambapo maofisa wake walisema yupo kwenye
vikao vya uongozi.
Yeyote aliyeguswa na habari hii na angependa
kumsaidia Amosi anaweza kuwasiliana naye kwa
simu namba 0765 765747 au 0715 756384.
MJUMBE BLOG tunapatikana mtandaoni kwa habari picha,Taarifa na Matangazo muhimu kila mara.
posted from Bloggeroid
Post a Comment