KAYA masikini 6,464 za wilaya ya Kilolo
mkoani Iringa, zimelipwa zaidi ya Sh Milioni 212.8 kwa kupitia awamu ya tatu ya
mpango wa TASAF zitakazowawesha kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia
mahitaji muhimu katika kipindi cha miezi miwili, Julai na Agosti, mwaka huu.
Kaya hizo kwa mujibu Mratibu wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Masikini Kilolo, Venance Mwaikambo ni kati ya kaya zaidi ya
31,000 za wilaya hiyo, zilizotambuliwa, kuhakikiwa na kuandikishwa katika
vijiji 70 kati ya vijiji 95 vya halmashauri hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Rukia
Muwango alisema zoezi la ulipaji wa fedha hizo lilifanyika kwa siku nne, Agosti
19 hadi 22, mwaka huu kwa vijiji hivyo ambavyo ni vya awamu ya kwanza ya mpango
huo.
Alisema serikali kwa kupitia mpango huo
inatoa ruzuku ya msingi na ya masharti kwa kaya masikini ili kugharamia
mahitaji ya msingi ikiwemo elimu, afya na maji.
Mratibu wa mpango huo, Mwaikambo alisema
ruzuku ya msingi inatolewa kwa kila kaya iliyoandiskihwa kwenye mpango ili
kugharamia mahitaji hayo ya msingi na ruzuku ya masharti nafuu inatolewa kwa
kaya masikini zenye watoto wenye umri wa kwenda shule na kliniki.
“Mpango unalenga pia kutoa ajira ya muda
kwa kaya hizo na zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi wakati wa kipindi cha
hari na majanga mbalimbali kama vile ukame na mafuriko,” alisema.
Mwikambo alisema kwa kupitia mpango huo
kaya masikini zitaboresha maisha yao kwa kupitia uwekaji akiba na shughuli za
kiuchumi kutoka kati ya Sh 20,000 na Sh 70,000 watakazokuwa wanapata kila baada
ya miezi miwili.
Mmoja wa walengwa wa mpango huo, Lickson
Chambaga (70) wa kijiji cha Luganga aliyepata Sh 20,000 kupiti mpango huo
alisema; “nitatumia fedha hizi nilizopata kuanzisha ufugaji wa kuku.”
Naye Anesi Malekala (66) wa Ikokoto alisema;
“Sh 40,000 nilizopata zitanisaidia mimi na wajukuu zangu wanne ambao ni yatima;
nitafuga kuku na faida nitakayopata nitanunua mbolea kwa ajili ya shambani.”
Kwa upande wake, Maimuna Kyando (48) mwenye watoto nane alisema amepata Sh 66,000 atakazotumia kukodi shamba katika msimu ujao wa kilimo ili azalishe mazao yatakayomuwezesha yeye pamoja na wanae kupata chakula.
Post a Comment