Unknown Unknown Author
Title: MAGGID MJENGWA:ASEMA;CCM INA PITIA KIPINDI KIGUMU MNO,VITA YA UKAWA KUGOMBEA MAJIMBO YATAJWA PIA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Ndugu zangu, Kesho vumbi la kampeni litaanza kutimka rasmi. Kwa uzoefu wangu wa kufuatilia siasa za nchi hii naziona is...
Ndugu zangu,
Kesho vumbi la kampeni litaanza kutimka rasmi. Kwa uzoefu wangu wa kufuatilia siasa za nchi hii naziona ishara za yatakayotokea. Kwanza kutakuwa na hali mbili zitakazojitokeza; Uhalisia na tamthilia. Kwamba mengine yatakuwa ni maigizo ya kisiasa. Ni bahati mbaya pia, kuwa tutarajie kushuhudia pia ushabiki wa kisiasa kwa mwenye kushabikia kushindwa kuuona uhalisia. Ni kwenye kutanguliza ushabiki ndipo mtu hupenda kusikia anachotaka kusikia, kuona anachotaka kuona. Ni vema na ni busara kwa mwanadamu, kuwa na ujasiri pia wa kusikia usichopenda kusikia, na kuona usichopenda kuona.
Mimi nitajitahidi kuyaangalia ya uhalisia. Ningependa msomaji nikusaidie pia kuyaona hayo ya uhalisia.
Ni uhalisia ninavyoandika sasa, kuwa CCM ina wakati mgumu kisiasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya uwepo wake.
Ni katika mazingira hayo, kuwa tutarajie, kuwa CCM itatumia nguvu ya chama chake kumsaidia kumnadi mgombea wake ambaye wana hakika atakubalika. Hivyo, kesho CCM hawatawatuma mgambo Jangwani kwenye uzinduzi wa kampeni zao; CCM watakwenda na makamanda wao. Tutarajie pia, kuwa hata wale wenye imani na CCM na ambao kwa kawaida huwa hawaendi kwenye mikutano ya CCM, kuwa kesho wengi wao hawatakaa kwenye mikeka au makochi yao majumbani wakiangalia runinga. Watainuka kwenda Jangwani kukipa sapoti chama chao.(P.T)
Ndio, mkutano wa kesho wa CCM Jangwani utatoa ishara za itakavyokuwa baada ya Oktoba 25. Na CCM ina historia ya kuendesha mikakati yake kwa kufuata mbinu za kijeshi. Walio kwenye ' War Room' ndani ya CCM, kesho ndio nafasi yao ya kuonyesha walivyojipanga. Kwa CCM, Mkutano wa Jangwani kesho ni ' Mama Wa Mikutano Yote Ya Kampeni'.
Maana, kihistoria, Dar es Salaam na muitikio wa Watu wa Dar es Salaam kujaa Viwanja vya Jangwani imekuwa ni kipimo cha namna chama kinavyokubalika. Hivyo, hatma ya Uchaguzi wa Mwaka huu inaweza kuamuliwa Jangwani.
Na baada ya hapo ni vita ya kwenye media kwa pande zote mbili. Atakayejipanga vema ana nafasi ya kuzoa kura nyingi pia.
Vinginevyo, uhalisia mwingine ni kuwa, kama ilivyo Kwa wavuvi, kuna mtego wa samaki unaitwa mgono. Ni aina ya tenga. Ni kubwa, pa kuingilia ni papana sana. Samaki anaweza kuingia kwenye mgono bila kujua kuwa anaogelea kwenye mgono. Hatimaye atafika mwisho na kuukuta upenyo mdogo.
Akivuka hapo samaki anaukuta mgono mwingine ndani ya mgono aliouacha nyuma yake. Na samaki akiogelea akafika mwisho, basi, mgono huo huwa umefungwa. Samaki hao watakuwa wameingia kwa wingi ndani ya mgono.
Na tabu ya samaki huwa hawana uwezo wa kuogelea kinyumenyume, na kwa kufuata utaratibu. Hivyo, samaki hao wote watakuwa wamenaswa kwenye mgono.
Kama mchambuzi wa habari na ninayefuatilia kwa karibu siasa za nchi hii, naliona kosa kubwa la wapinzani kuiga hata makosa yanayofanywa na CCM na hivyo wapinzani hao kujikuta wanaingia kwenye mtego wa mgono. Tunaona vita ya kugombania baadhi ya majimbo. Lakini, huko chini kabisa, wapinzani hawakupaswa kukaa Dar es Salaam na kuwachagulia wapiga kura madiwani wa kusiamama kwenye chaguzi.
Wapinzani walipaswa kujua, kuwa CCM bado ni chama chenye nguvu hata hii leo. Na uhalisia ni kuwa, hata kama Uchaguzi Mkuu ungefanyika kesho Jumapili, basi, CCM ndicho chama ambacho kingekuwa na wabunge wengi bungeni, na kingeunda Serikali.
Mwanasiasa anayeupuuza uhalisia huu hawezi kuwa mwanasiasa makini. Nchi hii inahitaji siasa za upinzani. Inahitaji uwepo wa wabunge wengi wa upinzani bungeni. Lakini, kazi kubwa inahitajika, na zaidi kujenga misingi ya vyama, si mijini tu, hata vijijini. Na kukubali kuwa, wapiga kura wa leo si wajinga. Wanahitaji uwepo wa Serikali himilivu- Stable Government. Na uhimilivu huo uanze kuonekana kwenye vyama vyenyewe na hususan kwenye demokrasia ya ndani ya vyama- Intra-party democracy.
Muhimu ni kuyaona sasa mapungufu na kuanza kazi ya kujisahihisha. Inawezekana.
Maggid.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top