Kilichomkera Zaidi Sumaye CCM, Alijeruhiwa Muda Mrefu
0Saa kadhaa zilizopita Tanzania imepokea habari nyingine kubwa zaidi ya kihistoria tangu kuanzishwa kwa vyama vingi baada ya waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kuwa waziri Mkuu wa pili kuhamia Upinzani mwaka huu.
Katika hotuba yake iliyooneshwa moja kwa moja kupitia vituo viwili vikubwa vya runinga nchini, unaweza kusoma katikati ya mistari na kugundua kuwa Sumaye alikuwa amejeruhiwa muda mrefu na CCM.Hivyo, uamuzi wake sio wa kukurupuka.
Wakati akizitaja sababu za kukihama chama tawala, Sumaye alisema kuwa amekuwa akionekana hana umuhimu wowote ndani ya CCM. Licha ya nyadhifa kubwa aliyowahi kuwa nayo, amejiona kama mwanachama wa kawaida kabisa wa chama hicho.
“Najua sina umuhimu wowote CCM. Mimi ni mwanachama wa kawaida tu. Naamini ninakoenda Ukawa nitakuwa na umuhimu na naamini CCM sasa wataona nilikuwa na umuhimu,” alisema Sumaye.
Jeraha jingine ambalo CCM walimpa Frederick Sumaye ni kufuatia onyo kali alilowahi kupewa na chama hicho ambalo anaamini hakutendewa haki na kwamba hata alipoomba kusikilizwa alipuuzwa.
“Nilipopewa adhabu ya onyo kali, sikupata nafasi hata ya kusikilizwa. Hata nilipokata rufaa walinipuuzia tu,” ni baadhi ya maneno ya Sumaye.
Waziri Mkuu huyo mstaafu alionesha kuwa CCM haikumtendea haki kama kiongozi wa ngazi ya juu kwa muda mrefu na kuwa uongozi wa chama hicho ulichukua maamuzi bila haki na kwa uonevu.
Sumaye ambaye jina lake pia lilikatwa na Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM katika mchakato wa kura za maoni kumpata mgombea urais mwaka huu, alisema kuwa ameamua kujiunga na Ukawa ili kuongeza nguvu zaidi ya kuiondoa CCM madarakani.
Sumaye alitoa wito pia kwa wanasiasa wengine wakongwe waliokuwa na ambao bado ni wanachama wa CCM waliofanya kazi katika ngazi mbalimbali za serikali, kujiunga na ngome ya upinzani ya Ukawa ili kusaidia katika kuongeza uzoefu wa kiutawala katika serikali ya awamu ya Tano ambayo anaamini itaundwa na Ukawa.
“Wale watu wenye nia njema waliowahi kuwa serikalini na nchi waje upinzani huku tuwasaidie hawa,” alisema.
Alikejeli mfululizo wa maneno ya vijembe yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa CCM, “Inawezekana kwa CCM mimi ni wale ambao wanaoitwa Makapi au Oil chafu.”
CCM imepanga kuzindua kampeni zake kesho katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam huku Ukawa wakiwa kimya wakidai bado wanatafuta sehemu nzuri zaidi itakayotosha ‘mafuriko’ wanayoyatarajia baada ya kukataliwa kutumia uwanja wa taifa.
Credit:Dar 24
Maelezo zaidi:
"Karibu Ndugu Frederick Sumaye katika mabadiliko ya kweli. Tushikamane na tusimame pamoja na wananchi kuongoza hamasa ya watanzania wanaotaka mabadiliko kwa kuiondoa CCM kupitia UKAWA. Hakuna anayeweza kusimama kuzuia nguvu ya umma katika kufanya maamuzi sahihi na magumu Oktoba 25, Mwaka huu. Karibu mpambanaji Sumaye".-Edward Ngoyai Lowassa

KAULI NGUMU ZA MH. SUMAYE ALIPOTANGAZA RASMI KUJIUNGA UKAWA:-
- "Hakuna mtu ambaye anaweza kufunga nadhiri na chama cha siasa"
- "Sina tatizo na mgombea wa CCM, nina amini hakuhonga na anachapa kazi,japokuwa ana mapungufu mengi katika nafasi hiyo"
- "Mwenyekiti alikuja na majina yake mfukoni, na yalikuwa yanafahamika,na mimi niliyafahamu"
- "Tatizo la rushwa katika chama cha mapinduzi wakati wa uchaguzi,limezidi"
- "Fedha nyingi zimetumika kwenye michakato ya urais, ubunge na udiwani"
- "Watoa rushwa wengi wametangazwa ndio wagombea wa ccm"
- "Maisha ya kuona hamna maisha nje ya ccm yamepitwa na wakati"

Post a Comment