Njonjo Mfaume
RAIS wa Afrika Kusini Jacob Zuma, alipotumia randi milioni 2.5 kujenga
bwawa la kuogelea kwa ajili ya familia yake, mpinzani wake, kijana
machachari, ambaye alipata kuwa kiongozi wa vijana ndani ya African
National Congress (ANC), Julius Malema, alimkejeli kuwa ametumia fedha
zote hizo za umma wakati yeye mwenyewe, Rais, na familia yake yote
hawajui kuogelea.
Malema, sasa kiongozi wa chama cha upinzani cha
kupigania Uhuru wa Kiuchumi (EFF) akaongeza kuwa rais wa kwanza wa
Afrika ya Kusini huru, Nelson Mandela, alijua kuogelea lakini hakujenga
bwawa la kuogelea la kiasi hicho cha fedha.
Tukatae, tukubali kuna
burudani katika kisiasa. Nenda popote duniani penye siasa za ushindani,
utasikia wanasiasa wakitoa hotuba na kauli za dhihaka, utani, vijembe na
kejeli dhidi ya wapinzani wao. Maneno ya namna hiyo huchangamsha siasa
na kufanya siasa kuwa si tu uwanda wa kujadili mambo makini yahusuyo
jamii husika na maendeleo yao lakini pia burudani ya aina yake.
Kule
Marekani, Rais Barack Obama anasifika kwa uwezo wake wa kurusha vijembe
vya dhihaka dhidi ya wapinzani wake. Wachambuzi wa siasa wanasema Obama
anatumia utani kama silaha ya kisiasa. Inaelezwa kuwa utani, dhihaka na
kebehi za Obama unakusudiwa si tu kukuburidisha lakini pia kuwaaibisha
wapinzani wake na hivyo basi kushawishi Wamarekani wamuunge mkono yeye.
Katika makala iliyochapishwa kwenye tovuti ya Shirika la Habari la CNN,
inaelezwa kuwa marais wengi wa Marekani wamekuwa wakitumia utani,
lakini si kwa kiasi alichofikia Obama.
Katika mlo na waandishi wa
habari za Ikulu ya Marekani mwaka 2011, Obama aliwaambia: “kuna watu
wanadai kuwa nimekaa kiprofesa (mwana taaluma) sana, sasa nataka
niwapangie vitabu vya kusoma ili baadaye muamue wenyewe kama madai hayo
ni ya kweli”.
Wiki chache kabla ya uchaguzi wa Marekani uliopita
Obama alimrushia mpinzani wake Romney kijembe kuhusu utajiri wake
akisema: “mapema leo nilienda kununua vitu madukani pale Midtown, lakini
naelewa kuwa Gavana Romney alienda kununua maduka pale Midtown”.
Tanzania nako burudani katika siasa zipo. Na huenda bila ya hizo, tusingekuwa hata na hamu ya kufuatilia hizo siasa zenyewe.
Namkumbuka marehemu mpwa wangu Mzee Rajab ambaye aligombea ubunge kule
Tunduru, mara kadhaa alikuwa akiwaambia wananchi katika kampeni zake
kuwa nyundo ambayo ni sehemu ya nembo ya CCM matumizi yake ni kuua
wananchi, kisha jembe ambalo nalo ni sehemu ya nembo hiyo ni kwa ajili
kufukia marehemu.
Pamoja na hamu yetu ya kuwasikiliza wabunge
wanaotoa hoja nzito na za kipekee, ziwe mbaya au nzuri kule bungeni,
Zitto Kabwe, Tundu Lissu, Freeman Mbowe, Hamisi Kigwangala na wengineo
tunafurahia pia kusikia waburudishaji, kina Joseph “Sugu” Mbilinyi na
Mwigulu Nchemba wakisuguana na kuchembana.
Binafsi kwa miaka kadhaa
nilipenda kuwasikiliza Mudhihir Mohammed Mudhihir aliyekuwa mbunge wa
Mchinga na John Magale Shibuda kutoka Maswa, si kwa sababu ya hoja,
bali uwezo wao kujieleza kwa lugha tamu zenye misamiati, vichekesho,
dhihaka, misemo, na, tamathali za semi.
Hivi karibuni, katika
Bunge la Katiba, utani, dhihaka, kejeli, kebehi, mbwembwe viliongezeka
maradufu. Hilo lilitegemewa maana kukusanya wajumbe zaidi ya 600,
wakiwamo wabunge wote, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wawakilishi
wa makundi mengine mbalimbali ya kijamii si mchezo. Mchanyato huo, wa
watu wengi wenye hulka, tabia na mitazamo tofauti, kama ni chakula
ungeweza kabisa kukusababishia maradhi ya tumbo kama si kuharisha.
Wapo baadhi yao walikwenda Dodoma wakijaribu kutumia nafasi hiyo kufanya
kila wawezalo ili kuonyesha utii kwa walio wateua na kuacha kumbukumbu
nzuri ya kudumu ili baadaye wafikiriwe katika nafasi za uteuzi mwingine.
Wapo pia wapinzani wa jadi kutoka kule Zanzibar, Cuf na CCM, ambao nao walijitahidi kutumia nafasi hiyo kuonyeshana ubabe.
Katika mkusanyiko huo mkubwa wabunge wa bunge hilo wakajikuta ‘ wame
overdose’ kejeli, kebehi, vituko na mbwembwe. Baada ya utani wa kawaida
tuliouzoea wa kisiasa ambao hata akina Obama wanautumia, wao
wakaboresha, dhihaka zikawa ni matusi pamoja na kauli za ubaguzi na
chuki.
Yupo mama mmoja, Asha Bakari, ambaye yeye alisema wazi kuwa
hakutokuwa na mabadiliko ya Serikali Zanzibar kwa njia za kidemokrasia
labda kwa njia za mapinduzi. Kisha, Mama Asha ‘akamchaaaamba kwelikweli’
na kumshambulia Ismail Jussa kwa mambo ya binafsi sana.
“Nasema
Zanzibar ni nchi ya kimapinduzi, na mie namwambia Jussa sasa, hatuitoi,
hatuitoi, hatuitoi, labda watupindue. Serikali ya kimapinduzi
haichukuliwi kwa karatasi. Hilo nawatanabahisha, na uwezo huo hawana
maana sisi ndio wenye madaraka”, Asha Bakari alirindima bungeni
akishangiliwa kwa vifijo na vigeregere.
“Zanzibar inaitwa Zenj
Empire, maana yake Zenj empire ni utawala wa watu weusi. Sasa mwanangu
Jussa jiangalie kutoka chini mpaka juu”, akaongeza mama Asha. Jussa ni
Mzanzibar aliyechanganya damu.
Nje ya Bunge, kulikuwa na Waziri
William Lukuvi ambaye akiwa amealikwa kama mgeni rasmi katika sherehe
moja ya kidini alitumia jukwaa hilo kusema mambo mengi ya hatari ikiwamo
kuwa ni muhimu Tanganyika iendelee kuidhibiti Zanzibar kwa sababu ina
Waislamu wengi na hivyo basi Waarabu watarudi na kutengeneza nchi ya
Kiislamu. Pia akaendeleza kutoa kauli za kutishia kuwa jeshi litapindua
nchi kama kukiwa na serikali tatu. Kutokana na kauli hizi za ubaguzi na
vitisho, wabunge wa upinzani walisusia bunge, hatua ambayo binafsi
sikuona kama ni ya busara.
Lakini, pamoja na kuwa upinzani ulikosea
kususia, kwa maoni yangu, jambo la ajabu zaidi ni kwamba CCM na serikali
yake haioni kuwa kuna tatizo katika kauli hizo. Adhabu za viongozi kama
hawa ilikuwa ni kujiuzulu tu.
Karibuni hapa, aliyekuwa makamu wa
raisi wa Kenya kati ya 2008 na 2013, Kalonzo Musyoka, ambaye kwa sasa ni
mmoja kati ya viongozi wakuu wa Muungano wa Upinzani wa Cord,
alilazimika kumpigia simu mwandishi wa habari kumuomba radhi baada ya
kukataa kujibu swali lake akimhisi ni mpinzani wa Muungano wao wa
kisiasa kwa sababu tu mwandishi yule ni Mkikuyu.
Mwandishi alianza
kuuliza swali lililoonekana likilaumu upinzani. Kalonzo akataka kujua
jina la mwandishi huyo na baada ya mwandishi huyo kumtajia jina, Kalonzo
akamwambia “Jina lako limekusaliti. Sina neno la kuongeza”.
Tukio
lile likageuka kuwa habari kubwa kuliko mada waliyowaitia wandishi.
Wabunge wa chama chake nao walijitokeza hadharani kumuombera radhi bosi
wao.
Tanzania kauli hizo za kibaguzi zinapita hivihivi. Hakuna
anayewajibika hata kwa kuomba radhi. Inawasaidia kisiasa, sasa kwa nini
wayakemee? Natamani CCM ambao ni mabingwa wa kuhubiri amani wangejua
kuwa moto mkubwa ulianza kwa cheche!
Ukichukua ile kauli ya mama
Asha Bakari, wakati fulani unajiuiliza hiki chama cha CCM ndicho kile
cha Mwalimu Julius Nyerere aliyesimama kidete kupinga ubaguzi wa rangi
Afrika Kusini? Bahati mbaya ni kwamba vyama vyote vya ukombozi
vimeserereka kimaadili. Juzi tu, Askofu Desmond Tutu amesema anashukuru
Mandela alikufa kuliko angeyashuhudia ya ANC ya sasa.
Kwa upande
mwingine wa shilingi, kuna Profesa Ibrahim Lipumba na kauli yake ya
Interahamwe. Katika kipindi ambacho nchi yetu iko katika uhusiano wa
mashaka makubwa na Rwanda, hakuna usaliti mkubwa kwa nchi yako kama
kuiita serikali na chama tawala Intarahamwe. Nadhani Lipumba alikosea
sana na labda naye angefikiria kuomba radhi.
Kuna burudani katika
siasa. Lakini siasa ni zaidi sana ya burudani. Siasa zinagusa maisha na
ustawi wa jamii ya watu, moja kwa moja kiuchumi na kijamii. Siasa
zinaamua mustakabali wa taifa. Ni siasa ndizo zimeifanya Korea ya Kusini
kuwa nchi tajiri na ile ya Kaskazini kuwa nchi masikini.
Kadhalika,
pamoja na kuwa kuna burudani ya malumbano ya kiushindani katika siasa
lakini malumbano hayo yasipozingatia hifadhi ya tunu za taifa za umoja,
usawa, heshima, utu – ni rahisi sana kuwa chanzo cha machafuko.
Nimalize kwa kunukuu kauli ya Zitto Kabwe aliyoituma katika ukurasa wake
wa facebook, anasema, “"vema basi viongozi wa dini zetu zote kuu,
Waislam na Wakristo, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wachukue wajibu wa kwanza, kuendelea kukemea vikali lugha za kibaguzi,
matusi na kejeli. Viongozi wa Bunge la Katiba wachukue jukumu la
kuwaadhibu wajumbe wanaotoa lugha za namna hii wakati wa mijadala na
viongozi wa vyama vya siasa waweke nidhamu kwa wanachama wao"
CHANZO:RAIA MWEMA
MJUMBE Sr