MGOMBEA
Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia anaungwa
mkono na vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, Edward Lowassa amesema
endapo atachaguliwa kuwa rais ataunda serikali isiyokuwa ‘nyoronyoro’.
Akiwahutubia
wananchi wa Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Shule
ya Msingi Bunju ‘A’, Lowassa alisema muda umefika kwa wananchi wa
Tanzania kufanya mabadiliko.
“Naombeni
mniteue niwe rais wenu ili mpate maendeleo ambayo hamkuwahi kuyapata
kwa kipindi cha miaka zaidi ya hamsini. “Mimi nitaunda serikali
isiyokuwa nyoronyoro na inayofanya kazi zake kwa ufanisi na kila
mtanzania ataweza kunufaika na rasilimali za nchi yake,” alisema Lowassa
aliyehutubia kwa takribani dakika kumi.
Alisema
endapo atafanikiwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano, serikali yake itafanya
kazi kwa spidi ya mwendo kasi wa 120 na hivyo lazima kutakuwa na
maendeleo makubwa kwa muda mfupi.
“Nitaondoa
changamoto zote zinazowakabili wananchi wa Tanzania, ikiwemo ukosefu wa
huduma ya maji safi na salama katika maeneo mengi hapa nchini,
nitatatua changamoto ya mazingira ya kufanyia biashara ndogondogo pamoja
na kutoa elimu bure,” alisema Lowassa.
Aidha,
aliwahakikishia wananchi kuwa wasiwe na hofu kuwa kura zao zitaibwa,
akisema, “Hakuna atakayeiba kura ng’o. Nimesikia kuwa kuna njama za
kuiba kura, hakuna jambo kama hilo, bali kila mtu akipiga kura
ahakikishe analinda kura hadi mwisho ili kutoruhusu mwanya wa kuiba na
hakuna atakayeiba kura ng’o.”
Awali,
akimkaribisha Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe
alisema wamezunguka katika baadhi ya maeneo ya nchi na kuona watanzania
wamechoka na ugumu wa maisha na hivi sasa wanataka mabadiliko.
“Watanzania
wanahitaji mabadiliko, tumepata mapokezi makubwa sana kila tulipopita
kuomba ridhaa ya wananchi, hii inaonesha ni jinsi gani wananchi hawa
wapo tayari kukombolewa,” alisema Mbowe.
Mbowe
aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura na kuchagua
Chadema ili kiwakomboe na kutatua changamoto zinazolikabili taifa. Baada
ya kutoka Kawe katika Manispaa ya Kinondoni, jioni Lowassa alikwenda
katika jimbo lingine la manispaa hiyo, Kibamba, kuendelea na mkutano wa
kampeni.
Post a Comment