Unknown Unknown Author
Title: WAJUMBE 201 WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA WAPIGWE MSASA.
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
  Dodoma. Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Haroub Mohamed Shamsi ameuomba uongozi wa chombo hicho kuangalia uwezekano wa kuwapiga msasa...
 
Dodoma. Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Haroub Mohamed Shamsi ameuomba uongozi wa chombo hicho kuangalia uwezekano wa kuwapiga msasa wajumbe 201 walioteuliwa na Rais ili wazifahamu kanuni.
Mjumbe huyo alisema kwa hali ilivyo sasa, wajumbe hao wamekuwa wakifunikwa na wajumbe ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Shamsi alitoa ombi hilo juzi wakati wa kupitia Kanuni za Uendeshaji wa Bunge hilo, kikiwamo kifungu kinachompa Mwenyekiti ‘rungu’ la kumkatisha Mjumbe anayerudia maneno wakati wa mjadala.
“Bahati mbaya sana tumeanza Bunge hili wakati hawa wajumbe 201 hatujawapatia mafunzo yoyote halafu tunawawekea kifungu hiki ambacho kiko `very harsh’ (kikali),” alilalamika mjumbe huyo.
Mjumbe huyo alipendekeza kuwa kabla ya Mwenyekiti hajamkatisha na kumtaka mjumbe aketi hasa kwa wajumbe hao 201, ni vizuri kwanza akamrudisha katika mstari.
“Kuweka kifungu hiki kwamba anapoanza kurudia mara ya kwanza tu akatishwe, nafikiri tutakuwa hatuwatendei haki hasa wale wa kundi la wajumbe 201,”alisema Shamsi.
Shamsi alisema wamewaomba viongozi wao wawasiliane na uongozi wa Bunge ili kuandaa utaratibu wa wajumbe hao kupigwa msasa baada ya kanuni hizo kupitishwa.
Shamsi alisema katika kipindi walichokaa ndani ya Bunge hilo, wameshuhudia majadiliano ya Rasimu ya Kanuni yakihodhiwa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Akijibu hoja hiyo kwa niaba ya Kamati ya Wajumbe 20 ya Kushughulikia Kanuni, Tundu Lissu alikiri kuwa kanuni hiyo ni kali lakini hawawezi kutunga kanuni mbili kwa ajili ya jambo moja.
“Ni kweli kuna wajumbe wapya na kama matakwa ya 35(4) yakichukuliwa yalivyo, yatawaumiza kwani ndio mara yao ya kwanza kushiriki kazi za kibunge,” alisema.
Lissu alisisitiza kuwa Bunge hilo haliwezi kulegeza kanuni hizo na kwamba yakitokea mazingira yanayotajwa na wajumbe hao 201, busara ya mwenyekiti itatumika.
Chanzo:Mwananchi leo
Na Mjumbe Jr
Mbozi

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top