Kingunge Ngombale Mwiru
MWANASIASA mkongwe na Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge
Ngombale – Mwiru, amesema makada wenzake wanaomshambulia aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba,
wanakitukana Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema kumtukana au kumshambulia Jaji Warioba, au wajumbe wengine wa
tume hiyo ni sawa na kukitukana Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza
serikali.
Kingunge alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akichangia sura ya
kwanza na ya sita ya rasimu ya Katiba, ambapo alisema wanaomshambulia
Jaji Warioba wanaonyesha utovu wa adabu, kwa kuwa chama kina maadili na
adabu katika kushughulikia masuala mbalimbali.
“Mimi sitakubali hata kidogo wajumbe watumie msimamo wa chama
kumshambulia Warioba au wajumbe wengine wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, si halali kumshambulia Warioba au mjumbe yeyote yule binafsi.
“Mimi ni Mwana CCM niliyeondoka madarakani siku nyingi lakini naamini
kuwa kumtukana mwenzetu ni sawa na kukitukana chama na sisi tuliopo
hapa, wanaomshambulia Warioba wanakosea sana, hapa tuna rasimu ya
Katiba ambayo ina mawazo tu, hakuna watu ndani ya rasimu hiyo, hatupaswi
kukiuka maadili kwa kuwatukana au kuwakashifu watu,” alisema.
Alisema kilichomo ndani ya rasimu ya Katiba si uamuzi wa mwisho,
hivyo wajumbe hawana sababu ya kumsema, kumtukana au kumkejeli mtu
yeyote aliyekuwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kingunge pia alitumia fursa hiyo kukemea lugha za matusi, vijembe na
kejeli zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wajumbe kwenye mijadala
mbalimbali.
“Hatuwezi kukaa hapa ndani kwa kudhalilishana, wale waliokuwa
wakitumia lugha hizo walikuwa wanatudhalilisha wote. Wengine walitumia
lugha hizo kwa waasisi wetu…Unyenyekevu ni sura moja ya msomi ambaye
ametumia fedha za Watanzania kupata elimu yake,” alisema.
Alisema wajumbe wamekwenda bungeni kuwatafutia wananchi wenzeo Katiba
mpya, iliyo bora na lazima izingatie miaka 50 ya muungano ambao
umekuwa na mafanikio makubwa.
“Katiba bora lazima iimarishe yale mafanikio tuliyoyapata katika
kipindi hicho ikiwemo muungano, umoja wa kitaifa, mshikamano, udugu na
kuunda mazingira ya amani na utulivu, kama haiimarishi, haifai hata
kidogo. Haya mafanikio yote yametokana na muundo wa serikali mbili
ulioasisiwa na wazee wetu,” alisema.
Hakuna Katiba bila UKAWA
Kingunge alisema kuwa ili Tanzania ipate Katiba mpya iliyo bora,
lazima kuwepo maelewano ya kuwashirikisha wajumbe wa Bunge hilo
wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Alisema kitendo cha wajumbe wa UKAWA kususia vikao vya Bunge,
kinaonyesha upungufu mkubwa walionao lakini Katiba mpya haitaweza
kupatikana bila ya wao.
Kingunge aliwaomba wajumbe wa UKAWA warejee bungeni kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandaa Katiba ya wananchi.
Alisema hata UKAWA wakirejea bungeni ni vema wajumbe wakatambua kuwa
kupatikana kwa Katiba mpya kunahitaji maridhiano ya pande hizo mbili.
“Hatuwezi kupata theluthi mbili ya kura hasa kwa wajumbe wa kutoka
Zanzibar watakaohalalisha maamuzi yetu bila kushirikiana na wenzetu,
lazima tuzungumze, theluthi mbili ni takwa la kisheria, hatuwezi
kulikwepa,” alisema.
Kingunge alisema kwa muda mrefu Zanzibar kulikuwa na mfarakano mkubwa
kati ya CCM na CUF lakini yalifanyika mazungumzo yaliyodumu kwa
takriban miaka 13.
“Tumezungumza kwa muda mrefu tangu 1998 lakini hatimaye tulibuni
suala la kugawana madaraka…katika hali ya Zanzibar tulisema haiwezekani
lazima tukubaliane, sasa Zanzibar imetulia. Ni kutokana na mazungumzo
hayo.
“Suala la Katiba mpya si utani ni lazima tukubali tuzungumze mpaka
tuelewane….humu ndani sisi wajumbe tuzungumze lakini na wakubwa huko nje
nao ni lazima wazungumze,” alisema.
UKAWA waliteka Bunge
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Makamu wa Pili
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Alli Idd, wamewataka
wajumbe wa UKAWA wabatilishe uamuzi wa kususia vikao vya Bunge Maalumu.
Kauli hizo walizitoa jana walipokuwa wakichangia sura ya kwanza na ya
sita za rasimu ya Katiba, ambapo walisema Katiba inayotungwa ni ya
Watanzania wote, hivyo ni vema UKAWA wakarejea bungeni.
Balozi Iddi alisema taifa limetumia fedha nyingi kugharimia ujenzi wa
Bunge Maalumu pamoja na kuwagharimia posho wajumbe wake ambapo mpaka
jana lilitumia zaidi ya sh bilioni 20, hivyo si busara kwa UKAWA kususia
vikao.
Alisema UKAWA ni sehemu muhimu katika utungaji wa Katiba na wajumbe
wake wametumwa na wananchi ambao wanataka matatizo yao yawekewe
utaratibu wa kushughulikiwa kwenye Katiba.
Alisema kutokana na umuhimu wa kutunga Katiba, Rais Jakaya Kikwete,
amekubali kuliongezea muda wa siku 60 zaidi Bunge hilo ambalo jana
limeahirishwa hadi Agosti 5, mwaka huu.
Alisema kuongezewa siku huko kumetokana na kutokamilisha kazi yake
kwa siku 70 zilizopangwa awali ambazo zimemalizika jana hivyo UKAWA
wanapaswa kutambua unyeti wa vikao vya bunge na umuhimu wao.
“Pamoja na serikali kutumia fedha nyingi kutengeneza ukumbi na
kulipana posho UKAWA wameamua kususia vikao vya Bunge. Nawasihi warudi
tuendelee na kazi hii tuliyopewa na wananchi. Katiba haitungwi
barabarani au kwenye mikutano ya hadhara bali bungeni.
“Nawasihi warejee bungeni tuifanye kazi hii tuliyotumwa na wananchi,
tumetumia fedha nyingi na tutaendelea kutumia, kila mmoja wetu analipwa
sh 300,000 kwa siku na serikali inatumia sh milioni 188 kwa siku kulipa
posho.”
Naye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema anaamini katika umoja, hivyo
kukosekana kwa wajumbe wa UKAWA ndani ya Bunge kumemsikitisha lakini
ataendeleza jitihada za mazungumzo nao.
Pinda ametoa rai hiyo wakati ni takriban wiki moja imepita tangu
alipokaririwa akitamba kuwa wanawafuata UKAWA huko huko kwa wananchi
kwenda kusema ukweli.
Pinda aliwasihi wajumbe wa UKAWA warejee bungeni huku akiwasihi
wajumbe wengine wajiepushe na lugha za kejeli na vijembe ambazo alidai
zimechangia mijadala kuwa katika mazingira magumu.
‘Mimi kila siku huwa nasema kuwa yaliyopita si ndwele…tugange yajayo,
naomba wenzetu UKAWA warejee bungeni, Katiba mpya inahitaji ushirikiano
wetu sote,” alisema.
Pinda pia alisema Tume ya Jaji Warioba imefanya kazi nzuri kwa kuwa
yapo mambo mengi ambayo hayamo kwenye Katiba ya sasa lakini
yameorodhoshwa kwenye Rasimu ya Katiba.
Alibainisha kuwa anapingana na rasimu hiyo katika eneo moja la muundo
wa serikali tatu kwa kuwa anaamini ni mzigo mkubwa kwa taifa na
litachangia kuvunja muungano.
Alisema kuwa wanaosema kuwa kutofuata mapendekezo ya tume ya Warioba
kwa kuwa imetumia fedha nyingi, wanakosea kwani wajumbe wa Bunge Maalumu
wamepewa fursa ya kuondoa, kuboresha na kuingiza mawazo wanayoona
yanafaa kuwemo kwenye Katiba mpya.
Naye Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, alisema kiti chake
kiliamua kuwaacha wajumbe wajadili kwa uhuru zaidi na wananchi waamue
kipi kinafaa.
‘Huko mitaani tunalaumiwa kwa kuwaachia wajumbe, sisi tulifanya hivyo
pasipo kutumia nguvu, kanuni au askari ili wananchi wajue tabia za
wajumbe wao na kuamua, tungebanana sana najua lazima tungepigana na
kutoana ngeu,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
MJUMBE Sr
Post a Comment