Unknown Unknown Author
Title: PAUL NONGA WA MBEYA CITY:MLIPUAJI WA MIAMBA ALIYE IBUKIA KWENYE SOKA! ADAI "SIMBA NA YANGA WAME HARIBU SOKA NCHINI" INGIA USOME ZAIDI!
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
  PAUL NONGA WA MBEYA CITY: SOKA WALA SI FANI YAKE SOKA imehama kutoka kwenye burudani na kugeuka kuwa chanzo kikubwa cha ajira du...

 
PAUL NONGA WA MBEYA CITY:
SOKA WALA SI FANI YAKE
SOKA imehama kutoka kwenye burudani na kugeuka kuwa chanzo kikubwa cha ajira duniani. Barani Ulaya wachezaji wamekuwa wakilipwa mamilioni ya shilingi kila wiki huku wengine wakinufaika na mikataba mbalimbali ya matangazo kutokana na umaarufu wao katika soka.
Kutokana na mabadiliko hayo vijana wengi kwa sasa wamekuwa wakijiingiza kwenye mchezo huo wa kuchezea ngozi ya ngombe yenye upepo ndani yake kwa kutumia miguu kwani imekua ni moja ya ajira inayolipa hapa nchini.
Mshambuliaji wa Mbeya City, Paul Nonga ni kati ya wachezaji walioingia kwenye soka huku akiwa ameacha kwa muda kazi aliyosomea kitaaluma. Nonga aliamua kufanya hivyo baada ya kuona fursa ya ajira kwenye mpira wa miguu.
“Mimi nimesomea mambo ya ulipuaji wa miamba hususani kwenye machimbo ya madini, hiyo ndio ilikua kazi yangu kabla ya kujiingiza rasmi kwenye soka la kulipwa, niliwahi kufanya hiyo kazi Mwadui ila nikaona hailipi.
“Baada ya kupata nafasi kwenye soka niliona ni bora niachane na hiyo kazi kwa muda kwani mpira umenipotezea muda sana tangu nikiwa nasoma hivyo niliamua tu kujiingiza moja kwa moja kwenye soka angalau linirejeshee fadhila kidogo,” anasema Nonga mzaliwa wa Shinyanga.
Nonga ambaye alikua akiichezea JKT Oljoro ya Arusha kabla ya kuhamia Mbeya City msimu huu anasema kuwa soka la Tanzania limeathiriwa na Simba na Yanga kiasi cha kupoteza ladha ya mchezo huo nchini.
“Simba na Yanga wameharibu soka nchini, hii ilikuwa kazi kubwa sana kwa timu yetu ya Mbeya City kuzijenga saikolojia za wachezaji kuepukana na kasumba hiyo na kuamini kuwa tunaweza kufanya vizuri hata zaidi ya klabu hizo kongwe nchini.
“Angalau kwa Mbeya City wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuondoa kasumba hizo lakini zimwi hilo bado linatesa timu nyingi zinazoshiriki Ligi Kuu Bara kwa kujiona wao ni wanyonge mbele ya timu hizo,” anasema Nonga anayevutiwa na uchezaji wa Mrwanda Didier Kavumbagu wa Yanga na Karim Benzema wa Real Madrid.
Nonga anaamini kuwa Mbeya City itakuwa na maisha marefu kwenye soka la Tanzania kwani ina mipango endelevu na viongozi wenye mtazamo wa mbali pamoja na sapoti ya mashabiki wa timu hiyo kuwa na moyo wa kujitoa kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya timu yao.
“Watu wanafikiri Mbeya imekuja kwa nguvu za soda, la hasha ni timu ambayo inatazama mbali, ukiangalia kwa sasa wana mipango ya kujenga uwanja na hosteli, hii itaifanya iwe timu iliyowekeza kwa maendeleo ya baadaye.
“Pia ukiangalia timu yetu imeweka kipaumbele kwenye soka la vijana kwa sasa, wakongwe tupo watano pekee huku vijana wakifurika kwenye timu, hii ni taswira kuwa timu itafika mbali,” anasema Nonga ambaye aliwahi pia kuichezea Rhino Rangers ya Tabora.
Mashabiki wa Mbeya City waliotapakaa maeneo mbalimbali nchini na wale wa Jiji la Mbeya wanaojitokeza kuishangilia timu hiyo katika michezo wanayocheza ndani na nje ya Mbeya wamemfanya Nonga kuamini kuwa sapoti hiyo ndiyo chachu ya mafanikio ya timu yao hadi sasa.
“Mashabiki wamekuwa ngao muhimu sana kwetu, tumekua hatuna mechi ya ugenini kwa maana kila tunapokwenda kucheza tunakuwa na nguvu kubwa ya mashabiki nyuma yetu, hilo linatupa faraja sana.
“Kama tusingekua na hii nguvu ni dhahiri kuwa tungekua na njia ndefu sana kufika hapa tulipo, mimi binafsi nawashukuru sana wakazi wa Mbeya kwa kuonyesha uzalendo kwenye timu yao,” anasema Nonga ambaye pia anapenda kucheza mpira wa kikapu.
Ujeshi wampeleka Mbeya
Nonga ambaye awali alikua akizichezea timu za jeshi za Rhino Rangers na JKT Oljoro anasema aliamua kutimkia Mbeya City ili kubadili maisha yake kwani alikuwa amekaa chini ya timu za jeshi kwa muda hivyo alitaka kupata changamoto mpya uraiani.
“Unajua mimi si mwanajeshi ila nilicheza kwenye timu mbili za jeshi mfululizo hivyo nilipopata nafasi ya kuhamia Mbeya ambayo ni timu ya kiraia niliona nafuu kidogo kwani ningepata changamoto mpya.
“Kwa sasa maisha ni mazuri ndani ya Mbeya, ni tofauti kabisa na timu nilizowahi kuzichezea awali kwani viongozi wako makini na wanatoa ushirikiano mkubwa kwa wachezaji,” anasema Nonga anayezipenda Real Madrid na Chelsea.
Malengo yake
Nonga anasema malengo yake kwenye soka kwa sasa ni kuisaidia timu yake kupata mafanikio zaidi kwenye misimu inayokuja, na pia kupata nafasi ya kucheza timu ya taifa na hata ikiwezekana kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
“Nimekuwa kati ya watu walioisaidia timu ya Mbeya kufika hapa ilipo nikisaidiana na kila mmoja mwenye majukumu kwenye timu hii, lengo langu ni kuisaidia timu ifike mbali zaidi ya hapa na hata kunyakua mataji mbalimbali,” anasema Nonga baba wa mtoto mmoja
“Nitafurahi siku moja pia nikipata fursa ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, nimejipanga kucheza kwa kujituma zaidi na kuongeza mazoezi ili niweze kufanikiwa katika hilo,” anaongeza Nonga.
 
MJUMBE Sr

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top