UKAWA WA SISITIZA HAWATA RUDI BUNGENI NG,OO!
Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu msimamo wao wa kutorudi bungeni kujadili Rasimu ya Katiba Mpya. Wengine ni wenyeviti wenza wa umoja huo, Profesa Ibrahim Lipumba (kulia) na James Mbatia. Picha na Michael Matemanga
Joto la Katiba Mpya linazidi kupanda nchini, huku baadhi ya wasomi na makundi mbalimbali ya watu wakizidi kutilia shaka utapatikanaji wa Katiba hiyo.
Mkurugenzi wa Shule ya Sheria ya Kenya (KSL), Profesa Patrick Lumumba na mwandishi wa habari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu wameonya kwamba kwa hali ilivyo hivi sasa hakuna Katiba Mpya inayoweza kupatikana.
Wakizungumza katika mdahalo uliohusu mivutano ya makundi katika mchakato wa Katiba Mpya jana jijini Dar es Salaam, walisema kuwa CCM haikuwa na nia njema tangu mwanzo, huku Rais Jakaya Kikwete akitajwa kushindwa kusimamia ipasavyo.
Profesa Lumumba alisema Katiba ya Tanzania imejaa viraka na kwamba inahitajika Katiba Mpya ambayo itakidhi matakwa ya Watanzania na karne ya 21, itakayokwenda sambamba na changamoto za Afrika Mashariki.(P.T)
Alisema nchi za Afrika Mashariki zilipata katiba zao kwa njia ya machafuko, hivyo Tanzania lazima itafute njia sahihi inayokubalika kwa wananchi wote bila ya kuwepo kwa kundi moja linalotaka kuhodhi mchakato wa Katiba Mpya.
"Tanzania ina nafasi ya pekee na kihistoria kujipatia Katiba Mpya bila vita na itakuwa ni jambo la kusikitisha ikiwa kwa mtazamo finyu ya kivyama utanyimwa na wanasiasa ambao fikra zao si za kukidhi matakwa ya katiba," alisema Profesa Lumumba.
Alieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete amekiri kuwa alifanya makosa katika kusimamia mchakato wa Katiba Mpya, hivyo Watanzania wanapaswa wamsamehe ili mambo yaende sawa.
"Nimesikiliza hotuba za Rais (Jakaya Kikwete) alikubali kwamba alikosea, tukumbuke Rais wa nchi hawezi akaja akapiga magoti, cheo chake cha rais hakikubali hivyo, akisema alitoa maoni kama mwananchi kile ambacho anasema ni kwamba nisameheni," alisema huku akishangiliwa na wajumbe ukumbini. Aliongeza kuwa iwapo Watanzania watataka Rais afanye jambo la ziada kuliko hilo alilofanya watashusha hadhi ya kiongozi huyo wa nchi.
Alisema Watanzania walipotunga sheria ya kufanya marekebisho ya katiba walifanya dhambi mbili za asili. Alizitaja dhambi hizo kuwa ni kuruhusu kuyataja baadhi ya mambo kwenye katiba kuwa ni matakatifu na kuvunja tume ya mabadiliko ya katiba.
"Mkiwa mnazungumzia mambo ya katiba hakuna mambo matakatifu yote lazima yazungumziwe. Tanzania siyo nchi ya kwanza Afrika Mashariki kutafuta katiba ni nchi ya mwisho," alisema huku akishangiliwa na wajumbe wa kongamano hilo.
Akiizungumzia dhambi ya pili alisema: "Lakini jambo ambalo halieleweki na wengi ni kwa nini Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Jaji Warioba (Joseph) iliyokuwa na uzoefu ikavunjwa ? Katika mataifa yote unaihifadhi tume mpaka mwisho."
Alisema tume hiyo ilitekeleza kazi yake kwa kiwango kikubwa na kwamba hakuna nchi Afrika iliyowahi kukusanya maoni kutoka kwa kila mwananchi.
Soma zaidi>>>>>>>>>
Post a Comment