Unknown Unknown Author
Title: KUHUSU KURA YA MAONI APRIL,30!
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Kujikwaa siyo kuanguka, bado tunaweza kubadili mawazo kwa maslahi ya Taifa Zikiwa zimesalia siku 42 kufika tarehe 1 Machi 2015, tarehe a...

Kujikwaa siyo kuanguka, bado tunaweza
kubadili mawazo kwa maslahi ya Taifa
Zikiwa zimesalia siku 42 kufika tarehe 1
Machi 2015, tarehe ambayo kwa mujibu wa
kifungu cha 5 cha Sheria ya Kura ya Maoni
ndiyo siku ambayo Asasi za Kiraia baada ya
kupewa ruhusa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
zitaanza kutoa elimu ya uraia juu ya Katiba
Inayopendekezwa. Kwa kawaida Elimu ya
Mpiga Kura hutolewa kila panapokuwapo
uchaguzi ama wa kitaifa kwa maana ya
uchaguzi wa Rais au katika ngazi ya jimbo
kwa maana ya uchaguzi wa ubunge na
halkadharika katika ngazi ya kata kwa maana
ya uchaguzi wa udiwani. Elimu ya mpiga kura
lengo lake hasa ni kumuandaa mpiga kura
kwa kumpa maarifa juu ya faida za kupiga
kura kama raia, namna ya kuwabaini
viongozi wazuri ambao anaweza kuwapa
dhamana kwa kutumia kura yake, lakini pia
elimu ya mpiga kura hugusa mambo mengine
muhimu kama vile utaratibu wa kupiga kura,
makatazo na jumla ni hamasa ya kujitokeza
siku ya upigaji kura.
Kwa upande wa Tanzania Bara kipindi hiki na
kama kweli bado Aprili 30 iko pale pale basi
Watanzania wanaoishi upande huu watapata
fursa ya kushiriki pamoja na Watanzania
wanaoishi Tanzania Zanzibar katika zoezi
adhimu, adimu na la kihistoria la Kura ya
Maoni. Kura ya Maoni ndiyo itakuwa hatua ya
mwisho katika mchakato wa kuandika Katiba
Mpya, siku hiyo raia wa Tanzania hasa wale
walioandikishwa katika daftari la kudumu la
mpiga kura watafanya uamuzi wa kuipitisha
au kutoipitisha Katiba Inayopendekezwa.
Kwa msomaji ambaye anasoma makala hii
kwa mara ya kwanza ni vyema akaelewa
hatua hii ya Kura ya Maoni imetanguliwa na
hatua tatu muhimu ambazo kwa mujibu wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 ni
Wananchi kote nchini kutoa Maoni yao
(Hatua ya kwanza), Wananchi kote nchini
kupitia mabaraza ya Katiba takribani 179 na
kuleta Watanzania 18,000 yale
yaliyosimamiwa na Tume ya Katiba na yale
yaliyoendeshwa na Taasisi mbalimbali zaidi
ya 600 na kuleta Watanzania zaidi ya milioni
nane (Hatua ya Pili), na Bunge Maalumu la
Katiba, ambalo pia lilileta pamoja wajumbe
zaidi ya 600 wakijumuisha wabunge wote wa
Bunge la Jamhuri, wajumbe wote wa Baraza la
Wawakilishi na wajumbe wengine 201 kutoa
Taasisi na asasi mbalimbali (Hatua ya Tatu).
Matarajio yangu ni kwamba zoezi kama hili
muhimu kabisa lapaswa kupewa uzito
linaoustahili. Kule Uingereza mwaka jana
(2014) walipiga kura ya maoni na tangazo la
siku ya kupiga kura lilitolewa mwaka mmoja
kabla yaani 2013. Hapa kwetu tangazo la
kupiga kura ya maoni limetolewa Mwezi
Oktoba Mwaka jana (2014) ikiwa ni miezi
saba kabla ya tarehe ya Kura ya Maoni.
Najaribu kulinganisha nchi hizi mbili kwa
maana kwamba kule Uingereza ambako
wenzetu wametangulia mbele karibu kwa kila
sekta ilionekana notisi ya mwaka mmoja
ingewatosha kwa wananchi wao kujua zoezi
lililo mbele yao, wawe na mjadala mpana na
wajiandae kisaikolojia na matokeo ya uamuzi
wao.
Waingereza wale hasa kule Uskochi waliona
mwaka mmoja kwa mazingira yao ungetosha,
na ninaposema mazingira yao nazungumzia
miundo mbinu kama barabara za kufika huku
na huko kufanikisha zoezi la Kura ya Maoni,
ninazungumzia mawasiliano ya kila namna,
redio, televisheni, magazeti ya kuchapa na ya
mtandaoni, matangazo mbalimbali na pamoja
na kuandaa utaratibu mzima wa kuendesha
kura ya maoni. Kwa hakika mwaka mmoja
uliwatosha na sisi tu mashuhuda kwamba
kura ile ya maoni kule Uskochi ilikwenda kwa
mafanikio makubwa, kwanza
walioandikishwa walikuwa wengi kifani
tofauti na matarajio ya wengi hasa hasa wale
ambao walikuwa wanapiga kura ya mara ya
kwanza, kundi la vijana na matineja.
Wananchi kule waliandikishwa kwa wingi na
kwa wakati, kisha kukawa na elimu ambayo
ilikuwa motomoto ambayo ilifuatiwa na
kampeni ya kukata na shoka kutoka kambi
mbili kubwa zilizojitanabaisha kama “Ndio
kwa Uskochi” au kwa Kiingereza “Yes
Scotland” wakitaka Uskochi Huru nje ya
Umoja wa Ufalme wa Uingereza (UK) na
kambi ile ya “Bora Kuwa Pamoja” au kwa
Kiingereza “Better Together” waliotaka
Uskochi iendelee kuwa sehemu ya Umoja wa
Ufalme wa Uingereza (UK).
Utaona natoa mfano huu wa Uskochi
nikifananisha na hapa kwetu, sina nia ya
kuiga kwasababu naheshimu sana ule usemi
niliojifunza kitambo kutoka kwa mshauri
wangu mmoja nadhani ni Dokta Maselle
Nzingula Maziku usemao “a leader does not
compare his or her success by comparing with
others but by the set goals prior set” yaani
“Kiongozi hapimi mafanikio yake kwa
kujilinganisha na wengine bali kwa malengo
aliyokwisha jiwekea awali”. Naheshimu pia
ule usemi usemao “tunajifunza kwa wengine”,
hivyo basi mfano wangu wa Uskochi
utufundishe kuona kama wenzetu walitenda
vile basi hata sisi kwa mazingira yetu
twaweza tenda kwa namna yetu pasina
kusahau uhalisia ni uleule.
Sasa tukirudi hapa nyumbani najiuliza na
nikitizama mazingira yetu, barabara zetu,
ukubwa wa nchi yetu yenye kilometa za
mraba zaidi ya 945,000 na mtawanyiko wa
wananchi wetu hasa wale wenye sifa za
kushiriki kupiga Kura ya Maoni. Maandalizi
ya teknolojia itakayotumika ile ya “biometric
Voter Registration” (BVR) ambayo ni ngeni
kabisa, teknolojia hii itatumika
kuwaandikisha wapiga kura kielektroniki,
zoezi hili si lelemama. Wananchi wetu
wanapaswa kuandaliwa kimaarifa juu ya
mfumo huu mpya utakaotumika
kuwaandikisha yasije tokea yale ya Malawi,
wao walipoanza ilileta shida kidogo, watu
wenye hila huwa hawakosekani katika jamii
yoyote ile. Hapa nazungumzia wale wenye
tabia za kujiandisha sehemu mbili au
wengine wajanja kwa hila watajiandikisha
hata sehemu tano, sijui wana uwezo gani,
sijui huwa wanapaa kutoka kituo kimoja
kwenda kingine au sijui ni uwezo mkubwa
wa bodaboda kwenda haraka, hata sijui.
Wajanja hawa wenye hila kwenye “BVR”
ndiyo mwisho wao. Kuna jamaa mmoja
mwingi wa porojo akaniambia wako wajanja-
hila wengine huvuka hata na majahazi
kwenda Zanzibar “kusaidia” kupiga kura
licha ya kwamba wao ni wakazi miaka nenda
rudi wa huku bara, wajanja-hila kama hawa
wanaweza kujikuta ni wakazi wa Bara lakini
wakapata kitambulisho cha kupiga kura
kutoka Zanzibar sasa unaweza “ukasaidia”
kura za maoni kule Zanzibar lakini kadri siku
zinavyokwenda utagundua haki zako za
kushiriki uchaguzi huku bara au eneo lingine
lolote halisi ukaikosa, kabla ya kuwa mamluki
naomba utafakari.
Sasa msomaji wetu, nakuuliza, ndani ya siku
42 zilizobaki kabla ya elimu kuanza, je,
tunaweza kuwaandikisha wapiga kura wote
takribani Milioni 20? Je, vile vifaa vya “BVR”
ambavyo baada ya majaribio vitakuwa
vimeshafanyiwa maboresho kule kiwandani,
vikarudishwa tena hapa Tanzania kwa
majaribio ya mwisho ili sasa kiwanda kifyatue
vifaa vyote zaidi ya 7000 ili zoezi liende bila
Changamoto tulizozibaini awali? Je, tuna
muda wa kutosha kutoa elimu ya namna ya
kujiandikisha hasa kwa kutumia huu
utaratibu na mfumo mpya wa uandikishwaji
wa “BVR”? Je, siku 42 tunaweza zaidi kwa
mazingira yetu na kupata mafanikio makubwa
kama yale ya wenzetu Uskochi? Najua kwa
wengine maswali yangu ni ya kipuuzi lakini
nikuhakikishie ni katika upuuzi dunia yetu
imepiga hatua, ni katika mawazo madogo
madogo tu, dunia ilibadilishwa na kuwa ilivyo
leo yenye tija, ugunduzi, ubunifu na
maendeleo tofauti na zama za mawe.
Natamani kweli mwanasiasa fulani ajitokeze
na ayaseme haya waziwazi maana ni kwa
maslahi ya Taifa, mwanasiasa huyo atakuwa
ameamua kusimama upande wa wananchi
katika kulinda Uhuru na Umoja wa Taifa letu,
natamani kumwona mwanasiasa huyo. Ndugu
Wananchi kama akikosekana basi, simameni
wenyewe na muwasaidie wanasiasa kujua
kuna maslahi ya nchi kwanza kisha maslahi
binafsi hufuata baadaye.



Tutembelee
MJUMBE BLOG mtandaoni upate Picha,Matangazo,Habari mpya,Taarifa muhimu kila mara.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top