MAJERAHA ya moto husababishwa na
mambo mbalimbali vikiwemo vyakula
mfano chai, maharage ama uji, umeme,
kemikali ama jiko la mafuta ya taa,
mkaa au gesi.
Kuungua kwa magari, nyumba na
maandalizi ya pombe za kienyeji pia
ni miongoni mwa mambo yanayoweza
kusababisha majeraha ya moto.
Majeraha hayo huwa ya aina tofauti,
yapo yaliyopo juu ya ngozi ambayo
hujulikana kama majeraha madogo, au
kiwango cha kwanza cha majeraha.
Kuna majeraha yaliyo ndani ndani ya
ngozi, huwa ni makubwa kiasi au
kiwango cha pili. Kwenye jeraha
kubwa ambalo ni kiwango cha tatu
hupenya safu zote za ngozi. Kiwango
cha nne cha jeraha la moto huhusisha
tishu zilizo ndani kama vile misuli
na mifupa.
Matibabu yake huzingatia ukubwa wa
jeraha. Lile dogo linaweza
kudhibitiwa kirahisi lakini jeraha
kubwa huhitaji utaalamu katika
zahanati, vituo vya afya au
hospitali. Majeraha ya kutoka ngozi
ni mengi kwa watoto chini ya miaka
mitano kwenye nchi nyingi, mengi ya
hayo husababishwa na watoto kugusa
vitu vyenye moto, kumwagikiwa na
vitu vyenye moto kama maji moto,
chai ama vyakula.
Wazazi nchini wenye watoto wenye
umri wa chini ya miaka saba
wameshauriwa wawe makini kuhusu
usalama wa watoto wao katika muda
huo wa ukuaji kwa kuwa mwaka moja
hadi miaka mitano huwa ni watundu,
hivyo wanakuwa katika hatari ya
kuungua.
Ushauri huo umetolewa na mwanafunzi
anayesomea masomo ya udaktari,
Tumaini Leandry katika ukurasa wake
wa mitandao ya kijamii. Maelezo yake
anasema, hospitalini nusu ya watoto
waliolazwa ni kutokana na kuungua
moto. Leandry anasema, wazazi
wanapaswa kuwa makini kwa watoto wao
na kuhakikisha wanakuwa mbali na
maji ya moto, uji, chai na mboga.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala
iliyopo Dar es Salaam, Dk Sophinias
Ngonyani anathibitisha kuwa ni kweli
idadi kubwa ya watoto chini ya miaka
mitano wanaungua kwa moto. Dk
Ngonyani anasema, tatizo hilo lipo,
ni kubwa katika hospitali hiyo.
Mtaalamu huyo anasema, watoto hao
wanaungua moto wa aina mbalimbali
mfano uji, maji ya moto, maharage na
chai vinapokuwa jikoni bila uangalizi
mzuri wa walezi ama wazazi. Kwa
mujibu wa Dk Ngonyani, watoto wenye
umri wa mwaka mmoja hadi mitano ndio
wanaopata ajali hizo.
“Sana sana ni watoto wenye umri wa
mwaka mmoja hadi mitano, kwa kuwa
umri huo ni watundu wanataka
kujifunza,” anasema. Ngonyani
anasema, wakati mwingine ajali hizo
zinatokana na uzembe wa wazazi ama
walezi wao. “Mara nyingine wazazi ni
wazembe au wanawaachia wadada
wazembe kulea watoto wao,” anasema.
Daktari huyo anasema, kama majeraha
hayo ni madogo mtoto hutibiwa kwa
siku chache, lakini kama mtoto
ameungua sehemu kubwa hulazwa kwa
muda wa wiki mbili hadi mwezi.
Anasema, kama mtoto atakuwa ameungua
sehemu kubwa sana humpatia rufaa ya
kwenda Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH) jijini Dar es
Salaam.
“Ukipata wagonjwa kama hao
wanachangia kujaza vitanda pasipo
sababu kwa kuwa ni uzembe uliofanywa
na mzazi ama mlezi, wakati
akiangaliwa vizuri tatizo hilo
huzuilika,” anasema. Anasema ,
kikubwa wanachokifanya wao kitaalamu
ni kutoa elimu ya ndani ya hospitali
kwa wazazi wa watoto hao haswa akina
mama ili tatizo hilo lisijirudie
tena kwa mtoto wake ama wa jirani
yake.
Pia huwashauri wanawake hao kuwa
mabalozi kwa wenzao wanaporuhusiwa na
kurudi nyumbani. Ngonyani anasisitiza
kuwa elimu wanayoitoa ni ndani ya
hospitali hivyo anaomba vyombo vya
habari na wadau wengine kushirikiana
katika kuelimisha jamii juu ya suala
hilo la moto kwa watoto wadogo.
Daktari bingwa wa watoto hospitalini
hapo, Irene Barongo anasema tatizo
la kuungua kwa watoto hao hutokea
zaidi msimu wa mfungo wa Ramadhani
kwa kuwa watoto wengi wanapelekwa
hospitalini hapo wakiwa na majeraha
ya moto. Daktari huyo anaeleza kuwa,
wakati mwingine nyakati za kuungua
kwa watoto wengi hubadilika
kutegemeana na msimu.
“Watoto hawa wamelazwa wodi namba
mbili wameungua kwa vyakula, chai,
maharage na uji. Hii ndiyo sababu
kubwa ya watoto kuungua ambao
wanaletwa hapa,” anasema daktari
huyo. Anasema, kwa mwezi hupokea
wagonjwa kati ya 30 na 40 ambao ni
watoto wadogo walioungua.
“Tunawapa wazazi ushauri. Tunatoa
ushauri kwa mama kwa kuwa ndiye
mlezi wa watoto kuwa anapokuwa
hayuko makini jambo lolote linaweza
kutokea. “Inabidi umakini kwa sababu
kuna kipindi mtoto anahitaji kufanya
kile mama yake anachofanya kama
kupika,” anasema Dk Barongo.
Anashauri majiko yawekwe mbali na
watoto na yasiwekwe katika maeneo
ambayo watoto wanapita. “Kwa mfano
wazazi wengi wamezoea kuweka majiko
yao karibu na mlango, maeneo hayo ni
hatari kwa kuwa ni njia ambayo
watoto huitumia,” Anasema, majeraha
hayo ya moto hupona kuanzia wiki
mbili au tatu kutegemeana na sehemu
ambayo kidonda kipo, kama ni maeneo
ya tumboni, au kwenye viungio
kidonda kinachelewa kupona.
Anasema , kuna dawa zipo ambazo
zinapatikana hospitali ila nyingine
wazazi wananunua wenyewe. Anasema
dawa za kukaushia kidonda kwa sasa
hazipo bohari ya dawa (MSD), ndiyo
maana wazazi wanatakiwa kuzinunua
kwa ajili ya matibabu ya watoto wao.
Mzazi Rahma Said mkazi wa Manzese,
Dar es Salaam anasema mwanawe
Khalifa Bakari mwenye umri wa miaka
mitatu na miezi minne aliungua na
sufuria ya maharage ya moto
iliyokuwa ukumbini. “Mtoto wangu
alidondokea sufuria Desemba 22 mwaka
jana, lakini sasa anaendelea
vizuri,” anasema.
Mzazi huyo anasema, dawa aina nne
amezinunua kwa ajili ya kumtibu
mtoto wake. Anashauri wazazi kuwa
waangalifu na kuwalinda watoto wao
kwa kuwa unapomlinda mtoto
inakupunguzia gharama za kukaa na
mtoto hospitalini pindi anapoungua.
Mwananchi huyo anasema, kutumia muda
mrefu kukaa na mtoto hospitalini
kuna athari kubwa kiuchumi kwa
familia kwa sababu, licha ya gharama
za tiba, mzazi pia anashinda kufanya
kazi za kumuingizia kipato. Mkazi
mwingine wa Dar es Salaam, Sia
Ramadhani anayeishi Kimara King’ongo
anasema, mtoto wake mwenye miaka
mitano, Aziza Nasir alipita karibu
na moto, nguo yake ikashika moto
akaungua.
Tukio hilo lilitokea Desemba 19
mwaka jana wakati amebandika maharage
jikoni. Anashauri wazazi na walezi
kuwaangalia watoto vizuri, wasicheze
ama kupita karibu na moto.
Anapongeza huduma nzuri hospitalini
hapo, lakini anaeleza kuwa wamekuwa
wakinunua dawa za matibabu kwa kuwa
hazipatikani hospitalini hapo.
Tutembelee MJUMBE BLOG Mtandaoni kwa Habari mpya,Picha,Matangazo,
Taarifa muhimu kila mara.
posted from Bloggeroid
Post a Comment