Michuano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika,
AFCON, inaendelea Jumatano katika hatua ya
nusu fainali kwa Ivory kupambana na
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Katika michezo yao ya robo fainali, Ivory Coast
iliwasambaratisha Algeria, kwa mabao 3-1.
Algeria ni timu nambari moja kwa viwango vya
ubora vya Fifa barani Afrika. Nayo Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo iliwaadhibu majirani zao
Congo kwa magoli 4-2.
Kiungo wa timu ya Ivory Coast Cheik Tiote
huenda akacheza mechi ya leo baada ya kupona
maumivu ya kifundo cha mguu, ambayo
yalisababisha akose mechi mbili za mwisho za
timu hiyo.
Kocha wa Ivory Coast, Herve Renard amesema:
“Tiote ameanza mazoezi mepesi. Itakuwa vigumu
kwake kuanza mchezo, lakini ameorodheshwa
katika kikosi cha leo.”
Naye kocha wa DR Congo Florent Ibenge
amesema hatapenda kumfanyia majaribio ya
kucheza mechi dhidi ya Ivory Coast, nahodha
Youssouf Mulumbu, ambaye kocha wake
amesema amepona kwa asilimia “70%”.
Mlinzi wa DR Congo Gabriel Zakuani hayumo
katika kikosi cha leo baada ya kuumia kifundo
cha mguu walipocheza dhidi ya Congo.
Alhamisi ni mtifuano mwingine wa nusu fainali
kati ya wenyeji Equatorial Guinea dhidi ya Ghana.
Kutinga hatua ya nusu fainali Equatorial Guinea
waliwang’oa Tunisia inayoshika nafasi ya pili kwa
ubora barani Afrika kwa mabao 2-1, huku Ghana
ikiichakaza Guinea magoli 3-0.
Post a Comment