Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini, imetoa siku 80 kwa uongozi wa
Chama cha Tanzania Labour (TLP)
kuhakikisha kinafanya uchaguzi wake wa
ndani wa kuwapata viongozi wapya.
Kauli hiyo imeitolewa baada ya baadhi ya
wanachama wa chama hicho kufikisha
malalamiko katika ofisi hiyo wakiiomba
itangaze kwamba uongozi wa Mwenyekiti
wa chama hicho, Augustine Mrema
umefikia kikomo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukweli na
Maridhiano wa TLP Taifa, Joram Kinanda
alimtuhumu Mrema kukiuka katiba ya
chama hicho, kuongoza chama kidikteta,
kuporomosha heshima ya chama na
kujilimbikizia madaraka.
Akizungumza ofisini kwake, Dar es Salaam
jana, Msaidizi wa Msajili wa Vyama vya
Siasa, Sisty Nyahoza alisema baada ya
kusikiliza pande zote zinazosigana ofisi
hiyo iliwataka viongozi kuandaa uchaguzi.
"Tuliwasikiliza wote upande wa Kinanda
na upande wa Mrema ambaye alikuwa na
sababu kwamba alishindwa kuitisha
uchaguzi kutokana na hali yake ya afya
lakini tumewaandikia barua kuwa ifikapo
Aprili 26 wawe wamekwisha kufanya
uchaguzi na si vinginevyo," alisema
Nyahoza na kuongeza: "Vyama hivi ili
viweze kujinasua na migogoro ya mara
kwa mara lazima vijiendeshe kama taasisi
na si chama cha mtu mmoja. Hii itasaidia
kukuza demokrasia nchini na siku zote
demokrasia inaanzia katika vyama vyetu
ndipo inakuja juu. kama vyama havina
demokrasia ni ngumu hata huku juu
kuwapo."
Post a Comment