Mkuu wa Mkoa akiwa na walinzi
wakeMWANZA: Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,
Magesa Mulongo, ambaye ni mwakilishi
wa Rais Jakaya Kikwete mkoani hapa,
amebuni aina mpya ya ulinzi wake
binafsi pamoja na msafara wa magari
unaoambatana naye anapokuwa katika
ziara zake za kikazi.
Aina hiyo ya ulinzi na msafara wake
wa magari unaofanana kwa kiwango
kikubwa na ule wanaopewa viongozi
wakuu wa kitaifa, akiwemo Rais na
Waziri Mkuu, ni wa kwanza
kushuhudiwa na wakazi wa mkoani hapa
na umedaiwa kugharimu kiasi kikubwa
cha fedha.
Msafara wake umekuwa ukiwajumuisha
pia askari wa usalama barabarani
ambao kazi yao ni kujipanga
barabarani na kuwazuia watumiaji
wengine wa barabara wenye magari ili
kusitisha kwanza safari zao mpaka
hapo Mulongo na msafara wake
wanapopita.
Katika msafara wake, Mulongo
huambatana na Mkuu wa Polisi wa
wilaya husika, maofisa usalama wa
wilaya na mkoa, magari kadhaa ya
watumishi wa Halmashauri ya Jiji la
Mwanza pamoja na maofisa wa wilaya
anazozitembelea.
Sambamba na msafara huo wa magari,
Mulongo pia analindwa na makundi
matatu ya wanausalama ambao ni
askari polisi wa kawaida, askari
kanzu na maofisa usalama wa taifa.
Ingawa amekuwa akitumia aina hii ya
ulinzi na usafiri hata katika safari
zake za kawaida asubuhi anapotoka
katika hoteli ya kitalii anayoishi
kwenda ofisini wake, katika ziara
yake ya kujitambulisha kwa wakazi wa
Mkoa wa Mwanza aliyoianzia Wilaya ya
Ilemela, ulinzi wake ulionekana
kuimarishwa zaidi, huku idadi ya
magari kwenye msafara wake nayo
ikiongezeka.
Watu wa makundi mbalimbali
waliozungumza na kuhusu aina hiyo
mpya ya msafara na ulinzi wa
Mulongo, wameeleza kushangazwa na
jinsi mkuu huyo wa mkoa
anavyojikweza na kudai kuwa una
chembechembe za vitisho.
Wakizungumza kwa sharti la majina
yao kutoandikwa gazetini kwa kile
walichodai kuwa ni kuhofia
kushughulikiwa na Mulongo, walisema
wana mashaka na mwenendo wa kiongozi
huyo na kubashiri kuwa unaweza kuwa
na athari mbaya kwa serikali na hata
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika baadhi ya maeneo ambayo
Mulongo alifika kujitambulisha na
kuzungumza na wananchi alionya kuwa
serikali itawachukulia hatua wale
ambao wamekuwa wakijitokeza kwenda
kulinda kura za wagombea wao nyakati
za uchaguzi.
“Nimekuja kwenu kujitambulisha kama
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, hilo ndilo
lengo la ziara yangu hii ambayo ni
ya kwanza tangu nifike mkoani hapa.
Nataka mtambue kuwa jukumu lenu la
kwanza ni kukomesha uhalifu,
niwasihi toeni taarifa za uhalifu
polisi. Lakini naambiwa na ninyi mna
tabia ya kubeba mawe na silaha za
jadi kwa madai ya kwenda kulinda
kura katika maeneo ya vituo vya
kupigia kura, sasa nawatahadharisha
kuwa watakaobainika na kukamatwa
watajuta na waliowatuma
tutawashughulikia,” alionya Mulongo.
Kabla ya kutoa onyo hilo, wakazi wa
Wilaya ya Nyamagana waliohudhuria
mkutano wa kujitambulisha
ulioitishwa na Mulongo, walitumia
fursa hiyo kutoa kero zao kwa
kumueleza kuwa wakazi wa maeneo ya
Bugando na Igogo wamekuwa wakivamiwa
na kuporwa mali zao na vijana wa
genge la kihalifu la Panya Road.
“Kuna wimbi la vijana wanaowavizia
watu nyakati za usiku na
kuwanyang’anya simu za mkononi na
wanawake wamekuwa wakikabwa na
kuchukuliwa mikoba na vito vya
thamani, tunaomba msaada wa askari
polisi kufanya doria maeneo
mbalimbali hapa Igogo ili kuondoa
kero hii,” alisema mmoja wa wakazi
wa maeneo hayo.
Baadaye Mulongo na msafara wake
walielekea Kata ya Butimba na
kuzungumza na wananchi katika eneo
la Stendi Kuu ya Mabasi ambako
alielezwa kuwa eneo hilo halina
miundombinu ya uhakika ya maji taka
na vyoo vinahitaji ukarabati.
Mmoja wa maofisa wa Halmashauri ya
Jiji la Mwanza, Mhandisi Ezekiel
Kunyaranyara, ambaye alitakiwa na
Mulongo kutolea maelezo suala hilo,
alisema taratibu za manunuzi ndizo
zinazochelewesha ukarabati huo,
lakini tayari mkandarasi yupo eneo
la stendi akiendelea na kazi.
Majibu hayo yalionekana kumkera
Mulongo, ambaye alimkaripia
Kunyaranyara kwa kumtaka asikilize
maagizo yake kwa sababu akiagiza
kitu lazima kitekelezwe haraka.
Alisema amehamishiwa mkoani Mwanza
kwa ajili ya kufanya kazi kwa
maelekezo maalumu, kwa hivyo
watendaji wasiotimiza wajibu wao
wajue watapoteza kazi.
Katika ziara yake hiyo, Mulongo
alitembelea Kata za Nyamagana,
Igogo, Butimba, Buhongwa, Mirongo,
Pamba na Igoma kwa upande wa
Halmashauri ya Jiji la Mwanza
(Nyamagana) na Ilemela alitembelea
Kata za Sangabuye, Bugogwa, Kirumba,
Pasiansi na Busweru.
Chanzo: Mabadiliko
Tunashukuru kwa kutumia huduma zetu.
Karibu tena.
Post a Comment